Kenya waandamana kupinga kupanda kwa bei

Wanachama wa mashirika ya kijamii pamoja na raia waliandamana katika miji mbali mbali nchini Kenya,kupinga kupanda kwa gharama za maisha.

Image caption mmoja wa waandamanaji

Hali hii imejiri baada ya bei ya mafuta kupanda wiki iliopita jambo ambalo limeathiri bei za bidhaa zengine muhimu.

Mjini Nairobi waandamanaji waliandamana kutoka uwanja maarufu wa Uhuru wakibeba mabango yenye ujumbe tofauti kusisitiza kilio chao.

''Tumeamua leo ni leo,njaa inauma hapa huku wakubwa wakiendelea kunona, sisi tumejitokeza kwa wakenya wote lazima watimize haki yetu, wakenya wanaumwa njaa hadi wanafariki dunia", alisema mmoja wa waandamaji.

Salama

Katika maeneo mengi maandamano yalikuwa ya amani huku polisi wakiongoza wale waliokuwa wakiandamana.

Mji wa Nairobi ambao kwa kawaida una matatizo ya foleni ndefu za magari,foleni ilikuwa ndefu zaidi wakati waandamanaji walipokuwa wanapita barabarani na mara nyingi polisi walisaidia kuweka barabara kuwa salama.

Ugumu wa maisha

Kwa zaidi ya saa moja walipita katika barabara za Nairobi hadi katika ofisi za waziri wa fedha,waziri mkuu,ofisi ya rais na kufikisha ujumbe wao bunge.

Mmoja wa wabunge aliahidi kuwasilisha malalamiko bungeni,''Nawahakikishia kwamba tuko pamoja naomba nipokee hayo malalamiko yenu na niwasilishe bungeni kwa niaba yenu'', Mbunge Ababu Namwamba aliahidi.

Raia hao pia walitaka waziri wa fedha Uhuru Kenyatta na mwenzake wa kawi Kiraitu Murungi kujiuzulu kwa kile walichokiita kushindwa kuwalinda wakenya na ugumu wa maisha.