Jonathan aelekea kushinda uchaguzi wa Urais

Raia wa Nigeria Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wa Nigeria

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais nchini Nigeria, yamebainisha kuwa rais wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, anaelekea kunyakua ushindi.

Huku idadi kubwa ya kura ikiwa imehesabiwa, Jonathan, ambaye ni Mkristu kutoka jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta wa Niger Delta, amezoa kura nyingi kuliko mpinzani wake wa karibu ambaye alikuwa mkuu wa majeshi wa nchi hiyo, Generali Muhammadu Buhari.

Generali Buhari anaungwa mkono na wapiga kura wengi kutoka eneo la Kaskazini mwa nchi hiyo, ambao wengi wao ni Waislamu.

Kufikia sasa rais Jonathan anaelekea kupata idadi ya kura inayaohitajika ya theluthi mbili ya majimbo yote 36 nchini humo.

Kiongozi wa kundi la waangalizi kutoka Muungano wa Afrika, rais wa zamani wa Ghana, John Kufuor, ameiambia BBC kuwa ameridhishwa na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria, Hassan Mhelela amesema kinachosubiriwa sasa ni kuona iwapo pande zote zitapokea matokeo hayo hasa kwa kuwa ushindani umekuwa mkali kati ya rais Goodluck Jonathan na mpinzani wake Generali Muhammadu Buhari.