Maelfu wakimbia machafuko Nigeria

Maelfu ya watu wamekimbia nyumba zao kaskazini mwa Nigeria baada ya ghasia kuzuka kufuatia kuchaguliwa kwa Rais Goodluck Jonathan.

Image caption Ghasia katika eneo la Kaduna

Shirika la Msalaba Mwekundu limeiambia BBC kuwa watu wapatao 16,000 wamekimbia makazi yao katika majimbo sita upande wa kaskazini, ambapo pia baadhi ya raia walilala katika kituo cha polisi kwa ajili ya usalama wao.

Bw Jonathan ametoa wito wa kumalizika kwa ghasia, na kutangaza hali ya kutotembea usiku.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ghasia katika eneo la Kano

Mpinzani wake mkuu, Jenerali Muhammadu Buhari, ambaye anatokea upande wa kaskazini, ameiambia BBC kuwa ghasia hizo zinasikitisha, hazina msingi na ni uhalifu.

Baadhi ya wanaofanya ghasia wanadai ulifanyika wizi wa kura, lakini kiongozi huyo wa zamani wa kijeshi amesema anataka kutojihusisha yeye na chama chake katika ghasia.

"Katika saa 24 zilizopita, kumekuwa na ghasia nchini: hii imehusisha kuchoma moto kanisa na inasikitisha, na pia haikuwa na ulazima," amesema katika taarifa yake.

"Lazima nisisitize kuwa kinachotokea sio suala la kikabila au la kidini."

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Machafuko Kano, Kaskazini mwa Nigeria

Bw Jonathan, anayetokea upande wa kusini, alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais wa Jumamosi, huku tume ya uchaguzi ikisema alipata takriban 57% ya kura milioni 22.5 zilizopigwa, na Jenerali Buhari akipata kura milioni 12.2.

Waangalizi wa kimataifa wamesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.