Wajane wa India wapigwa mpaka kufa

Image caption Ramani ya India

Wajane wawili wa kike wamepigwa mpaka kufa na mtu mmoja katika jimbo la Haryana lililopo kaskazini mwa India.

Polisi ilimkamata mtu mmoja mwenye umri wa miaka 23, mpwa wa mmoja wa wanawake hao. Alikuwa katika kifungo cha nje baada ya kutumikia kifungo cha gerezani kwa makosa ya ubakaji.

Walioshuhudia waliwaambia polisi alimwuua shangazi yake na mwanamke mwengine huku wanakijiji wote wakishuhudia, baada ya kuwashutumu kuwa katika uhusiano wa mapenzi ya jinsia moja.

Haryana ni eneo lenye msimamo mkali sana na lenye mfumo dume.

Waandishi walisema kile kinachoitwa "kujiua kwa heshima" ni jambo la kawaida eneo hilo.

Walisema kumekuwa na matukio kadhaa kwenye eneo hilo la kijiji la Haryana ambapo wanawake na wanaume wanaokana mila na heshima za kifamilia hutengwa, huuliwa au hata kuuliwa kiholela hadharani.

Mauaji ya hivi karibuni yalifanyika siku ya Jumapili katika kijiji cha Ranila.

Iliripotiwa kuwa anayeshutumiwa alianza kumpiga mwanamke mojawapo, aliyetambulika kwa jina la Suman mwenye umri wa miaka 35, na rungu la mbao baada ya kumshutumu kuwa na "uhusiano usio wa kawaida" na shangazi yake Shakuntala.

Dakika chache baadae, alimburuta shangazi yake kwenye mitaa ya kijiji hicho na kumpiga mpaka kufa mbele ya wanakijiji wote waliokuwa wakiogopa kuingilia, waandishi walisema.

Wawili hao walitoka damu mpaka kufa huku wanakijiji wakiangalia.

Afisa wa polisi alisema, "Aliwatishia wanavijiji wengine kutowasaidia wajane hao na hata kuita madaktari."

Alisema aliwaua wanawake hao kulinda "heshima ya familia."