Malema wa ANC afikishwa mahakamani

Mkuu wa jumuiya ya vijana wa Afrika Kusini wa chama cha ANC, Julius Malema, amefikishwa mahakamani mjini Johannesburg katika kesi inayohusu chuki iliyoleta mvuto wa hali ya juu.

Jumuiya ya Waafrikaana inataka Bw Malema azuiwe kuimba wimbo wenye utata uliokuwa ukitumika zama za ubaguzi ukiwa na maneno "wapige risasi makaburu".

"Boer" yaani makaburu inamaanisha wakulima kwa lugha ya Waafrikaana na wanasema kutumia maneno hayo kunachochea chuki za kibaguzi.

Image caption Bw Julius Malema

Bw Malema alianza kutoa ushahidi wake akisisitiza kuwa yeye si mgomvi, na wimbo huo usichukuliwe kwa uhalisia wake.

Waendesha mashtaka walisema kama kiongozi wa African National Congress Bw Malema ana wajibu wa kuzungumza kwa niaba ya watu na hilo ndilo limesababisha " watu Kushikwa na wasiwasi kwa kila unalosema na unalofanya."

Bw Malema amekana kuwa "huleta utata."

Mamia ya watu walikuwa nje ya mahakama kuu kushuhudia kesi hiyo yenye mvuto, inayoonyeshwa kupitia televisheni kubwa kwa wale waliokaa nje.

Watu muhimu kutoka chama hicho cha ANC waliojitokeza mahakamani kumwuunga mkono Bw Malema walisema wimbo huo ni sehemu ya historia ya ANC, sehemu ya mapambano yao, alisema mwandishi wa BBC Karen Allen ambaye alikuwa nje ya mahakama hiyo.