Michael Owen ahuzunishwa baada kuomewa

Mshambuliaji wa Manchester United, Michael Owen amesema amehuzunishwa sana kutokana na kuzomewa na mashabiki wa Newcastle siku ya Jumanne, walipotoka sare ya 0-0 katika uwanja wa St James' Park.

Owen mchezaji wa zamani wa Newcastle, alizomewa alipoingia katika dakika ya 81.

Owen amesema katika mtandao wa Twitter: "Kupata mapokezi mabaya ukiwa nje ya uwanja wa nyumbani inakera sana. Inakufanya ujitahidi ufunge bao!"

Aliongeza: "Nilifahamu nitazomewa kama wanavyofanya mashabiki wengi, lakini iwapo wangefahamu ukweli basi wangekuwa na mawazo tofauti."

Owen alijiunga na Newcastle akitokea Real Madrid kwa kitita cha paundi milioni 16 mwaka 2005 na alifanikiwa kufunga mabao 30 katika mechi 79 alizoshiriki.

Mshambuliji huyo wa England jitahada zake hazikuweza kufua dafu mwaka 2009 kuiokoa Newcastle isiteremke daraja na akaihama klabu hiyo na kujiunga na Manchester United akiwa mchezaji huru.

Baada ya mchezo wa siku ya Jumanne, Owen, mwenye umri wa miaka 31, alijibu mapigo ya kuzomewa na mashabiki wa Newcastle, akisema: "Kwa kile ambacho nyinyi mashabiki wa Newcastle mnachokisema, mfurahi kwamba niliondoka katika klabu! Iwapo ningefahamu mapema, basi ningeondoka mapema zaidi!

"Mkiangalia rekodi yangu, nilijitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu kuitumikia Newcastle. Chini ya KK (Akimaanisha Kevin Keegan) nilicheza vizuri sana na sitasahau mechi tuliyoshinda 2-1 dhidi ya Sunderland tarehe 20 mwezi wa Aprili 2008.

"Ninapokutana na mashabiki wa Newcastle au wa Liverpool wote wanaheshimu niliyofanya katika klabu zao. Uwanjani wanabadilika, mmoja anaanza kuzomea wengine wanafuata.

"Hata hivyo siombi huruma. Mradi familia yangu hawanizomei ninapopita mlangoni, sijali kitu!!!"

Owen alitazamia mapokezi ya kukera katika uwanja wa St James' Park, akasema kabla ya mchezo: "Ni siku nzuri, jua linawaka hapa Newcastle! Najiandaa kukutana na marafiki wangu wa zamani lakini mashabiki watanipokea kwa mtazamo mwengine!"

Matokeo ya mechi hiyo yameifanya Manchester United kupoteza nafasi ya kuongeza wigo wa pointi katika msimamo wa ligi kileleni.