Wenger kufanya mabadiliko

Kwa mara ya kwanza kabisa kocha wa Arsenal Arsene Wenger amekiri kuwa kweli anahitaji kufanya mabadiliko ya kikosi cha klabu yake.

Image caption Arsene Wenger

Wenger ameyasema hayo siku ambapo Sir Alex Ferguson amesema kuwa kitisho kinayoikabili klabu yake ya Manchester united ni kutoka Chelsea iliyopiga hatua.

Wenger amesema kuwa klabu ya Arsenal ina msimamo mzuri kifedha na ikibidi tunaweza kufanya mabadiliko makubwa.

Aliongezea kuwa, katika ulimwengu wetu kila mmoja analia hana fedha, lakini mtu asiyetumia pesa atakuwa ni mjinga.

Wenger amesema kuwa nia yao ilikuwa kujenga uwanja mpya bila kupoteza nafasi kileleni mwa Ligi kuu ingawaje walifahamu kuwa watakuwa na kipindi kigumu cha mda wa miaka minne hadi mitano.

Kwa hiyo tulichukuwa uwamuzi wa jinsi ya kusalia miongoni mwa timu bora tukitegemea mapato duni yaliyopo.

Tumejitahidi, lakini sasa hivi, bila shaka watu wamechoka. Ninaelewa vyema kwa sababu hata mimi nimechoshwa pia.

Ukitizama msimu wetu utaona kuwa hatuhitaji mabadiliko makubwa. Hapo tutakosea tukifanya hivyo.

Ukiwa na biashara ya gazeti lililo katika nafasi ya pili bora kwa mauzo, hufungi biashara yako.

Lakini lazima tuzingatie dunia ya sasa ambapo ukimaliza wa pili kwa tofauti ndogo, kila mmoja atakuona kama taka.

Akizungumza na wandishi wa habari baadaya mechi ya Manchester United dhidi ya Everton, Wenger aliuliza Je hisia zangu zinanisukuma katika soko? Nahisi daima kuna haja ya kuimarisha kikosi.

Shinikizo la kushindwa kupata ufanisi kwa msimu wa sita mfululizo lilionekana kumdhuru Arsene Wenger siku ya jumatano aliposhuhudia vijana wake wakishindwa kuzuia kuporomoka kwa uongozi wa magoli matatu kwa moja.

Mfano wake wakati akifuatilia pambano hilo umetajwa 'kama adhabu' na wadadisi, akiwemo mwandishi wa gazeti la sportsmail Graham Poll.

Alimsimulia mwandishi huyo kuwa ana nia ya kuongezea majina makubwa kwenye kikosi chake, wachezaji kama Leighton Baines na Per Mertesacker, ambao wana uwezo wa kuifanya klabu ya Arsenal ibuni kikosi kilichoimarika zaidi.

Meneja wa Manchester United Ferguson anakubali kuwa kweli Aresenal kuimarisha kikosi chake kwa kuongezea wachezaji walio na uzowefu kuimarisha kikosi chake.

Ferguson aliongezea kusema kuwa ingawa Arsenal ina wachezaji walio bora kuliko Chelsea lakini ratiba inaonesha kuwa Chelsea wana michuano rahisi kuliko ya Arsenal.

Miongoni mwa wachezaji wanaotazamiwa kuondoka, Denilson atakuwa wa kwanza kuondoka baada ya klabu hiyo kumtangaza kwa kuweka bei ya pauni milioni 5 kwa mcheza kiungo huyo.

Wachezaji Gael Clichy na Nicklas Bendtner huenda wakafuata Mbrazil huyo. Mabadiliko haya ya kipindi cha soko bila shaka yatawaridhisha mashabiki wa Arsenal ambao wamejawa na uchungu pamoja na kukerwa na matokeo ya kushindwa mara kwa mara na miaka sita bila mafanikio.

Hata hivyo, Wenger ameonya kuwa sera yao imekuwa kukuza vipaji vyao wenyewe kwa sababu hawana uwezo wa kuwasajili akina Ronaldo.