Watu 57 wameuwawa mapigano Sudan Kusini

Katika vita baina ya jeshi la serikali na wapiganaji wakati Sudan Kusini inapojitahidi kupambana na uasi katika eneo hilo.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Raia wa Sudan Kusini

Serikali ya Sudan Kusini inajitahidi kupambana na uasi wakati nchi hiyo inajitayarisha kujitenga na Sudan Kaskazini, ambapo uhuru unatarajiwa mwezi wa Julai.

Mapigano yalizuka baina ya jeshi la Sudan Kusini na wapiganaji wake wa zamani waliokuwa wakisubiri kujumuishwa kwenye jeshi la jimbo lenye mzozo la Jonglei.

Zaidi ya wapiganaji 55 waliuwawa na wanajeshi na raia 70 walijeruhiwa.

Idadi hiyo huenda ikaongezeka, maelezo yakitolewa.

Sudan kusini inajaribu kuzima uasi wa vikundi kama saba vya waasi, huku inakaribia uhuru kamili katika miezi mitatu ijayo.

Umoja wa Mataifa unasema watu zaidi ya mia nane wameuwawa na 94,000 wamelazimika kuhama makaazi yao tangu Januari.

Mzozo huo unatia wasiwasi kuhusu mustakbali wa taifa hilo jipya.

Katika siku za karibuni, watu wamehamishwa kutoka jimbo muhimu la mafuta la Unity, baada ya mapigano ya siku nne.

Sudan Kusini imeishutumu serikali ya Sudan Kaskazini, kwa kuwasaidia wapiganaji wa kusini, madai ambayo yamekanushwa na kaskazini.