Bw Mubarak apelekwa hospitali ya Cairo

Image caption Bw Hosni Mubarak

Aliyekuwa Rais wa Misri, Hosni Mubarak, anatarajiwa kupelekwa kwenye hospitali ya kijeshi mjini Cairo baada ya daktari kutangaza kuwa afya yake inamruhusu kusafiri.

Amekuwa hospitalini huko Sharm el-Sheikh tangu aanze kuumwa wakati wa kuhojiwa juu ya madai ya kuhusishwa na rushwa na mauaji ya waandamanaji.

Waendesha mashtaka walisema Bw Mubarak mwenye umri wa miaka 82 alitakiwa kupelekwa hospitali ya magereza ya Tora, lakini haikuwa tayari kumpokea.

Baraza la kijeshi lililoshikilia madaraka mwezi Februari linashinikizwa kumshtaki.

Watoto wawili wa kiume wa Bw Mubarak, Gamal na Alaa, pamoja na maafisa wengine waandamizi na wafanyabiashara walio karibu naye tayari wameshikiliwa kwenye gereza la Tora.