Amesty:Nchi za kiarabu zatumia nguvu kuzima maandamano

Nembo ya Shirika la Amnesty International
Image caption Nembo ya Shirika la Amnesty International

Serikali ambazo hazipendi demokrasia zinafanya mafanikio ya kihistoria ya kutafuta uhuru na haki katika nchi za kiarabu kuwa katika hatari,shirika la Amnesty International limesema.

Wakichapisha ripoti yao ya kila mwaka, shirika hilo la kutetea haki za binaadamu linataja mbinu moja ni kung'ang'ania kudhibiti teknolojia ya mawasiliano.

Wameshtumu serikali za Libya, Syria, Bahrain na Yemen kwa kulenga kushambulia maandamano ya amani ili kuendelea kukaa madarakani.

Na pia wanasema nchi zenye utawala mbaya kama vile China, Iran na Azerbaijan zimejaribu kuzuia mapema matukio kama hayo ya watu kutetea haki zao.

Kundi hilo la wanaharakati limetoa ripoti yake ya dunia kufwatia miezi kadhaa ya maandamano katika mashariki ya kati na kaskazini mwa Afrika.

Marais waliokuwa madarakani kwa muda mrefu wa Tunisia na Misri waling'olewa,lakini viongozi katika mataifa mengine wamejaribu kukabiliana na maandamano kwa kutumia mbinu za kuafikiana kisiasa pamoja na kutumia nguvu.