Arsenal yazinduka yailaza Man United 1-0

Arsenal imefanikiwa kuifunga Manchester United iliyopwaya katika mbio za kuwania ubingwa ambao kwa sasa umebakia wazi wakati vinara wa ligi Manchester United wakiwazidi kwa pointi tatu Chelsea walio nafasi ya pili huku ikisalia michezo mitatu.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Aaron Ramsey akishangilia bao na Va Persie

Mwamuzi Chris Foy alishindwa kuona mpira wa wazi uliochezwa kwa mkono na Nemanja Vidic kipindi cha kwanza akiwa katika heka heka za kuokoa krosi ya Theo Walcott, huku Robin Van Persie akijiandaa kuudonoa kwa kichwa.

Ingawa Manchester United walikuwa nusura wasawazishe kwa mkwaju wa free-kick wa Wayne Rooney, lakini kwa ujumla Arsenal waliendelea kuumiliki mchezo.

Bao la Arsenal lilipatikana katika dakika ya 56 baada ya Aaron Ramsey kuunganisha vyema pasi aliyosogezewa na Robin Van Persie.

Iwapo mabingwa watetezi Chelsea watashinda katika uwanja wa Old Trafford siku ya Jumapili ijayo, wataongoza ligi kuu ya England.

Arsenal wanazidi kujichimbia nafasi ya tatu wakiwa na pointi 67.

Katika mechi za awali Liverpool imejisogeza hadi nafasi ya tano ya msimamo wa ligi baada ya kupata ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Newcastle.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Maxi Rodriguez akishangilia bao lake la kwanza

Liverpool walimiliki mchezo hasa dakika za mwanzo na iliwachukua dakika 10 kupata bao la kuongoza lililofungwa na Maxi Rodriguez.

Newcastle United walijitahidi kuibana Liverpool na katika dakika ya 59 Mike Williamson alimchezea rafu Luis Suarez na wenyeji wakazawadiwa mkwaju wa penali ambapo Dirk Kuyt hakufanya ajizi na kuukwamisha mpira wavuni na kuiandikia Liverpool bao la pili.

Suarez alikamilisha uhondo wa mabao kwa wenyeji alipofunga bao la tatu. Andy Carroll mchezaji wa zamani wa Necastle aliyechukuliwa na Liverpool, aliingia zikiwa zimesalia dakika 20 kabla mchezo kumalizika.

Matokeo hayo yameinyanyua Liverpool hadi nafasi ya tano wakiwa pointi 55 sawa na Tottenham waliosukumwa hadi nafasi ya sita, lakini wakipishana kwa wingi wa mabao.

Nayo Wolves ilikosa nafasi ya ya kupanda kutoka timu tatu zilizo chini kushuka daraja, baada ya kutoka sare na Birmingham waliocheza wakiwa 10.

Image caption Steven Fletcher akishangilia bao lake

Steven Fletcher aliipatia Wolves bao la kwanza kwa mkwaju wa penalti baada ya Ben Foster kumchezea rafu Stephen Ward dakika ya saba ya mchezo.

Sebastian Larsson aliachia mkwaju uliogonga mwamba na baadae akafanikiwa kuisawazishia Birmingham kutokana na kichwa hafifu cha kuokoa alichopiga Michael Mancienne.

Kwa matokeo hayo Wolves wanaendelea kubakia nafasi ya 19 na pointi 34, huku Birmingham wakifanikiwa kubakia nafasi ya 15 na pointi 39. Bado wasiwasi wa kushuka daraja watakuwa nao iwapo hawatafanya vyema kwa michezo iliyosalia.