Uingereza yamfukuza balozi wa Libya.

Waandamanaji nje ya makaazi ya Kanali Gaddafi Haki miliki ya picha Reuters

Balozi wa Libya nchini Uingereza amefukuzwa kufuatia kushambuliwa kwa ubalozi wa nchi hiyo mjini Tripoli.

Balozi za kigeni katika mji mkuu zimelengwa na makundi ya watu wenye ghadhabu kufuatia ripoti kuwa ndege za kivita za shirika la NATO zilimuua mwana wa kiume wa mwisho wa kanali Muammar Gaddafi, Saif Al-Arab Gaddafi.

Waandishi wa BBC nchini Libya wanasema ubalozi wa Uingereza umeteketezwa moto.

Waziri wa mashauri wa nchi za kigeni William Hague amesema kuwa utawala wa kanali Gaddafi umeshindwa na jukumu lake la kulinda ubalozi huo na kwamba balozi Omar Jelban amepewa saa 24 kuondoka nchini Uingereza.

Wakati huo huo, Umoja wamataifa umetangaza kuwa utawaondoa wafanyikazi wake wa kimaifa kutoka mjini Tripoli baada ta vifaa vyake katika mji huo pia kushambuliwa na makundi ya watu wenye hamaki.

Katika mji wa Misrata, mji pekee unaoshikiliwa na waasi ulioko magharibi mwa Libya, wanajeshi watiifu kwa serikali wameshambulia eneo lililoko karibu na bandari, usiku wa kuamkia leo.

Uingereza sasa haina balozi katika mji mkuu wa Libya, Tripoli.