Bondia mkongwe Henry Cooper afariki

Bingwa wa zamani wa uzito juu mkongwe Sir Henry Cooper, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 76 nyumbani kwa mwanawe Oxted, Surrey.

Image caption Sir Henry Cooper

Bingwa huyo wa Uingereza, Jumuia ya Madola na Ulaya, alipigana mara 55 na anakumbukwa sana katika pambano lake la mwaka 1963 alipomsukumia konde lililomuangusha chini Muhammad Ali - wakati huo akiitwa Cassius Clay.

Katika taarifa yake, Ali alisema amempoteza "rafiki yake wa zamani", akimuita, "mpiganaji hodari na muungwana".

Cooper aliyezaliwa London, aliwahi kushinda tuzo ya Mwanamichezo Bora wa mwaka mara mbili, alitunukiwa cheo cha Sir mwaka 2000.

Pamoja na mabondia wengine hodari wa Uingereza akiwemo Frank Bruno, Tommy Farr na Lennox Lewis, Cooper anaaminika ni bondia hodari Uingereza kuwahi kumpata katika uzito wa juu.

Baada ya kucheza ngumi za ridhaa ikiwemo michezo ya Olympiki ya Helsinki mwaka 1952 akiwa na umri wa miaka18, Henry na pacha wake George, aliyefariki dunia mwaka jana, wote waliamua kujiunga na ngumi za kulipwa wakiwa na umri wa miaka 20 mwaka 1954.

Aliendelea kucheza kwa mafanikio katika ngumi za kulipwa, lakini hakuwahi kushinda taji la dunia hadi alipostaafu akiwa na umri wa miaka 36, mwaka 1971 baada ya kutwangwa na Joe Bugner mwaka mmoja baadae baada ya kutangazwa na BBC kuwa ameshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa Mwaka mara mbili, mwaka 1967 na 1970.

Cooper, atakumbukwa sana kutokana na mapambano yake mawili na Ali miaka ya 1960.

Alimuangusha chini kwa konde zito la kushoto lililopewa jina la jina 'Enry's 'Ammer - ukiwa ni umaarufu wa konde lake la kushoto - lakini Ali baadae akashinda pambano hilo lisilokuwa la ubingwa mwaka 1963 katika uwanja wa Wembley.

Ali baadae alizungumza kupitia televisheni ya Uingereza kwamba Cooper "alinipiga ngumi kali hadi wazee wangu Afrika nao wamepata habari".

Akielezea juu ya kifo cha Cooper, Muhammad Ali amesema, "ameishiwa maneno ya kusema" kutokana na kifo cha rafiki yake.

"Henry kila wakati alikuwa na sura ya kutabasamu kwangu; ni tabasamu ya unyeyekevu na upendo", alisema Ali. "Ilikuwa ni jambo jema kuwa karibu na Henry. Nimempoteza rafiki yangu wa zamani. Alikuwa ni bondia hodari na muungwana."