Calderon: Mourinho anaidhuru Real Madrid

Rais wa zamani wa Real Madrid Ramon Calderon, amesema haiba ya klabu hiyo imeharibiwa kutokana na tabia za Jose Mourinho wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Ubingwa wa Ulaya dhidi ya Barcelona.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Jose Mourinho

Real imetolewa katika mashindano hayo na mahasimu wao wakuu wiki hii, lakini mechi baina ya timu hizo zilikumbwa na vitendo vya utovu wa nidhamu kutoka kwa mashabiki, wachezaji na maafisa wa klabu.

Mourinho alitolewa nje katika mchezo wa awali baada ya kupinga kadi nyekundu na baadae matamshi aliyoyatoa yakamletea matatizo zaidi.

"Kuzungumza namna ile kumeidhuru Real Madrid," Calderon aliiambia BBC kitengo cha michezo.

Hasira zilizozuka wakati wa mapumziko katika mchezo wa awali wakati kulipokuwa na kutoelewana kwenye mstari wa unaougawa uwanja, wachezaji walipokuwa wakitoka uwanjani, zilisababisha mlinda mlango wa Barcelona Pinto kuoneshwa kadi nyekundu.

Real baadae ikawalazimu kucheza wakiwa 10 mara tu baada ya kipindi cha pili kuanza, baada ya Pepe kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kumchezea vibaya Dani Alves.

Mourinho ilimlazimu kujiondoa mwenyewe katika eneo wanalokaa makocha, baada ya kuonekana akitamka mbele ya mwamuzi wa akiba kwa kebehi "mmefanya vizuri."

"Ni wazi kabisa dhidi ya Barcelona huna nafasi," alitamka Mourinho. "Sielewi kama ni matangazo kwa Unicef [wafadhili wa fulana za klabu ya Barcelona], Sifahamu ni kwa sababu ni wazuri sana, lakini wanazo nguvu hizi.

Kauli na tabia za vilabu vyote viwili zilisababisha Uefa kuwashtaki mahasimu hao wakuu katika soka ya Hispania.

Bodi ya nidhamu na udhibiti ya Uefa itasikiliza mashauri ya timu hizo siku ya Ijumaa tarehe 6 Mei.

Mpambano wa marudiano uliofanyika siku ya Jumanne ambapo timu hizo zilifungana bao 1-1 na kuifanya Barcelona kuingia hatua ya fainali kwa mabao 3-1, pia kulikuwa na visa.

Wakati huu, Mourinho hakushiriki.

Wachezaji wa Madrid walielekeza hasira zao kwa waamuzi, baada ya Gonzalo Higuain bao alilofunga kukataliwa, na klabu hiyo huenda ikakabiliwa na mashtaka zaidi.

Winga wa Real Cristiano Ronaldo alisema: "Mwakani huenda Barcelona wakapewa kombe moja kwa moja."

Lakini Calderon ameshutumu tabia za wachezaji na meneja wa Real Madrid.

"Klabu kubwa hazipaswi kumlaumu mwamuzi kwa makosa yao au kufungwa kwao," alisema Calderon.

"Tumewekeza paundi milioni 400 katika kipindi cha miaka miwli iliyopita kuwa klabu muhimu sana na imara, kwa hiyo unapopoteza mchezo usitafute kisingizio cha majeruhi, hamkuwa na bahati, waamuzi au jambo lolote lile. Iwapo umeshindwa unapaswa kuwapongeza wapinzani wako, basi.

"Alichokifanya Mourinho kuzungumzia Uefa na waamuzi hakikubaliki kabisa."