Mkutano kuhusu Libya unafanyika Italia

Mazishi ya mwanawe Gaddafi baada ya kuawa a NATO Haki miliki ya picha AFP

Kundi la kimataifa kuhusu Libya, maarufu kama Contact Group, linakutana leo mjini Roma, Italia kujadili mzozo nchini humo.

Italia itatumia mkutano huo kupendekeza njia za kutatua mzozo huo, kama vile kuweka makataa ya kuendelea kwa shughuli za kijeshi nchini Libya.

Msaada kwa waasi nchini Libya pia utajadiliwa.

Muungano huo wa kimataifa kuhusu Libya unajumuisha washirika wa Muungano wa NATO, mataifa ya kiarabu na makundi mengine.

Ikiwa ni majuma 11 tangu mzozo huo uanze, muungano huo una maswala mengi ya kujadili.

Miongoni mwa maswala yatakayo jadiliwa ni iwapo kundi hilo litatoa msaada kwa waasi walioko mashariki mwa nchi, upatao dola billioni 3 , ili waweza kulipia dawa, chakula na vifaa vingine.

Huenda wakaafikiana kuhusu jinsi ya kuwasaidia kwa muda. Pia, huenda wakajadili vipi waasi wanaweza kuanza kuuza mafuta ili waweze kujifadhili.

Italia pia inataka kutafuta njia ya kuweka makataa kwa shughuli za kijeshi zinazoendelea. Wanachama wengine wa kundi hilo huenda wakaona vigumu kukubali pendekezo hilo hasa wakati mzozo huo ukionekana bado haujapata suluhu.