Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Polisi matatani

Wanakijiji nchini Bangladesh wamewashikilia mateka polisi, wakiwatuhumu kwa kufanya wizi. Wakazi wa kijiji cha Dinajpur wamesema watu sita walivunja nyumba moja katika kijiji hicho kaskazini mwa Bangladesh na kuiba fedha na dhahabu. Ingawa watu hao hawakuwa wamevaa nguo za polisi, lakini wanakijiji wamesema waliwatambua.

Wezi hao walipojaribu kutoroka kwa kutumia gari, wanakijiji hao waliwafukuza na kuwakamata. Hasira ziliongezeka baada ya polisi mwenzao kufika na kutaka kuwaokoa wenzake.

Inadaiwa alifyatua risasi hewani, lakini hata hivyo na yeye aliwekwa chini ya ulinzi. Kundi jingine la wanakijiji hao walikishambulia pia kito cha polisi na kukichoma moto. Sakata hilo lilitulia, baada ya maafisa wa ngazi za juu wa polisi walipowasili, na kuwasimamisha kazi askari wanaotuhumiwa.

Abiria wenye hasira

Nchini Argentina, wasafiri walichoma moto treni ya abiria, kutokana na huduma za usafiri kucheleweshwa.

Abiria hao kwanza walimtupa nje dereva wa treni hiyo pamoja na msaidizi wake, baada ya kushindwa kuvumilia kucheleweshwa kwa safari yao.

Makumi kadhaa ya abiria walihusika katika sekeseke hilo, lililotokea karibu na mji mkuu wa Argentina, Buenos Aires. Polisi wa huko wamesema pia baadhi ya wasafiri walifanya uharibifu katika ofisi ya kuuzia tiketi, kwenye kituo hicho cha reli.

Usingizi juu ya mti

Wanunuzi katika mtaa mmoja wa biashara nchini Uchina walipatwa na mshangao wakati waliposikia sauti ya mtu akikoroma bila ya kumuona.

Taarifa kutoka Lanzhou, kaskazini mwa Uchina zinasema hatimaye waliona mahala sauti inapotokea, baada ya kumuona mwanamama mmoja akiwa kalala fofofo juu ya mti.

"Yaani tusingejua sauti inatokea wapi, kama sio kiatu chake kimoja kuanguka" amesema mmoja wa wanunuzi katika eneo la soko. Polisi hatimaye walifanikiwa kumuasha na kumshawishi mwanamama huyo kuteremka kutoka juu ya mti huo wenye urefu za futi ishirini, baada ya kumuahidi kumpa chakula na maji.

Gerezani bila kujijua

Afisa mmoja wa jiji nchini Ujerumani amemuokoa mkazi mmoja wa huko aliyejikuta kaingia ndani ya gereza bila kujijua.

Bwana huyo aligutuka na kukuta tayari yuko ndani ya gereza la wanawake. Shirika la habari la reuters limesema, meya wa jiji la kaskazini la Hildesheim alisikia kelele za kuomba msaada,

wakati akipita karibu na gereza hilo, na kutoa taarifa kwa polisi mara moja. Polisi walifika na kumwachilia huru bwana huyo mwenye umri wa miaka ishirini na nne. Bwana huyo aliwaambia polisi kuwa alikuwa akifanya matembezi, bila kujua kuwa ameingia ndani ya gereza, na mpaka alipogutuka akakuta tayari geti la gereza limefungwa.

Polisi wamesema wanalifanyia uchunguzi suala hilo, na kutazama kwa nini lango la gereza liliachwa wazi, na hata mtu. tena mwanaume kungia ndani.

Bi harusi akimbia mume

Bwana harusi mmoja nchini Italia amemfikisha mahakamani msichana aliyekuwa akitazamia kumuoa, baada ya bi harusi huyo kubadili mawazo katika dakika ya mwisho.

Shirika la habari la ABC limesema bwana huyo mwenye umri wa miaka thelathini na miwili, amefungua kesi ya madai, na anataka kulipwa Euro laki tano. Bi Harusi amesema alibadili mawazo ya kuolewa baada ya kupendana na mwanaume mwingine muda mfupi kabla ya harusi yake.

Bwana harusi huyo amesema amepatwa na athari za kihisia, na mali, kwani tayari alikuwa ameandaa fungate nje ya jiji la Roma, na pia katika visiwa vya Pasifiki.

Shirika la habari la Italia ANSA, limesema bwana huyo aliyejulikana kwa jina moja tu la Ricardo, alikuwa tayari kanisani akimsubiri mke wake mtarajiwa, kabla ya kuambiwa kuwa mke huyo amebadili mawazo, na kuwa hatafika kanisani na hivyo kulazimika padre kukatisha misa ya ndoa.

Kichanga chasajiliwa kucheza soka

Klabu moja ya soka ya Uholanzi imemsajili mtoto mwenye umri wa miezi kumi na minane.

Klabu hiyo ya jiji la kusini la Venlo imemsajili mtoto huyo ambaye alipata umaarufu kupitia picha zake zilizooneshwa kwenye mtandao wa youtube. Radio Netherlands imeripoti kuwa mtoto huyo Baerke van der Meij alipata umaarufu baada ya baba yake kuonesha picha za mtoto huyo akipiga mpira kwa ufundi na ustadi mkubwa.

Hata hivyo uhalisi wa picha hizo za video haujathibitishwa. Klabu iliyomsajili inaitwa VVV Venlo imempa mkataba wa miaka kumi. Babu wa mtoto huyo aliwahi pia kuichezea klabu hiyo. Nafasi atakayocheza mtoto huyo bado haijafahamika. Hata hivyo taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo ya soka imesema huenda akachezea upande wa kulia kwa sababu mashuti yakya mguu wa kulia yalionekana kuwa na nguvu na ufundi mkubwa.

Na kwa taarifa yako

Binadamu anaweza kufa haraka zaidi kwa kukosa usingizi kuliko kukosa chakula.

Tukutane wiki ijayo... Panapo Majaaliwa...