Nafasi ya nne iko wazi, West Ham bado

Matumaini ya Manchester City kucheza Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, umeingia dosari baada ya kulazwa mabao 2-1 na Everton ambao walikuwa nyuma hadi kipindi cha kwanza.

Haki miliki ya picha PA
Image caption Leone Osman

Manchester City ndio wa kwanza kufunga bao kipindi cha kwanza kwa mkwaju mkali wa Yaya Toure.

Sylvain Distin aliisawazishia Everton kwa kichwa baada ya kuunganisha mkwaju wa free kick uliochongwa na Mikel Arteta na mlinda mlango Joe Hart alishindwa kuokoa mpira ulioonekana si wa hatari sana.

Baadae Everton wakionana vyema walifanikiwa kupata bao la pili lililofungwa kwa kichwa na Leon Osman baada ya kuunganisha krosi ya Phil Neville.

Matokeo hayo yameibakisha Manchester City nafasi ya nne wakiwa na pointi 62, huku Everton wakisalia nafasi ya saba na pointi 51.

Katika mchezo mwengine mabao ya Shola Ameobi na Steven Taylor yaliipa Newcastle ushindi dhidi ya Birmingham waliocheza wakiwa 10 huku wakiendelea kusalia katika eneo baya la kuteremka daraja.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Shola Amoebi

Ameobi alifunga kwa mkwaju wa penalti baada ya Liam Ridgewell kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Chris Foy kwa kuuokoa mpira kwa mkono uliokuwa ukielekea wavuni ambao ulipigwa kwa kichwa na Fabricio Coloccini.

Taylor baadae akaongeza bao la pili na kuifanya Newcastle waongoze kwa mabao 2-0.

Lee Bowyer aliipatia Birmingham bao la kufutia machozi kabla ya mapumziko.

Matokeo hayo yameipatia Newcaste pointi 44 wakiwa nafasi ya 10, huku Birmingham wakibakia nafasi ya 16 na pointi 39.

Wigan imeendelea kupigana kiume kuepuka kushuka daraja baada ya kwenda sare ya 1-1 na Aston Villa ambao kwa sasa wamepata ahueni ya kutoteremka daraja.

Image caption Ashley Young

Charles N'Zogbia alikuwa wa kwanza kuipatia Wigan bao baada ya kazi kubwa iliyofanywa na Victor Moses kuwapangua walinzi wa Aston Villa.

Lakini Ashley Young aliisawazishia Aston Villa kwa mkwaju wa yadi 22 kutoka langoni.

Mkwaju wa Hugo Rodallega nusura ungeipatia Wigan bao la pili, kabla ya Darren Bent kukosa nafasi nzuri ya kupata bao baada ya mkwaju wake karibu na lango kuokolewa na mlinda mlango wa Wigan Ali Al Habsi.

Wigan wameendelea kusalia nafasi ya 17 na pointi 36, Aston Villa wakiwa wamekusanya pointi 42 wakijikita nafasi ya 14.

Bao la kujifunga mwenyewe la Zat Knight liliipatia ushindi Sunderland dakika za mwisho dhidi ya Bolton. Sunderland imeshinda kwa mabao 2-1.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Sulley Muntari

Baada ya mkwaju wa Daniel Sturridge wa Bolton kugonga nguzo, Boudewijn Zenden alifanikiwa kuipatia Sunderland bao la kuongoza kabla ya mapumziko.

Sturridge alikosa nafasi nyingi za kuipatia Bolton mabao kabla hajapumzishwa na nafasi yake kuchukuliwa na Ivan Klasnic aliyeipatia Bolton kwa kichwa dakika tatu kabla mpira kumalizika na Bolton wakijua kwamba mpira utakiwisha kwa sare.

Lakini Sulley Muntari alikimbia na mpira na kuachia mkwaju langoni kwa Bolton na ukamgusa Knight aliyeshindwa kuondoa kabla haujavuka msatari langoni na kuiandikia Sunderland bao la pili.

Na bao la dakika za mwisho la kusawazisha lililofungwa na Thomas Hitzlsperger, liliipatia pointi moja West Ham waliokuwa wakicheza dhidi ya Blackburn, lakini bado West Ham wanabakia kuburura mkia wa Ligi Kuu ya England.

Image caption West Ham hatarini kushuka daraja

Rovers walipata bao la mapema katika dakika ya 12 lililofungwa na Jason Roberts kwa mkwaju mkali karibu na lango.

West Ham walionekana kukata tamaa hadi Hitzlsperger aliporudisha uhai kwa kufunga bao la kusawazisha kwa mkwaju aliopiga umbali wa yadi 20.

Na nusura West Ham wangepata bao la pili lakini nafasi hiyo ikapotezwa na Robbie Keane akiwa karibu kabisa na lango.

Bado ligi haijamalizika lakini kuna kila dalili na ishara kwamba West Ham watakuwa na kazi kubwa ya kuhakikisha hawateremki daraja msimu huu.