Wakimbizi zaidi ya 400 waokolewa

Wakimbizi hao walikuwa kwenye boti iliyogonga mwamba katika kisiwa cha Lampedusa na watawasili Lampedusa tarehe 8 Mei walinzi wa mwambao walisema.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boti ya wakimbizi

Picha kwenye televisheni zilionesha baadhi ya wakimbizi wakiruka kutoka kwenye boti na kuanguka baharini.

Wengine walionekana wakining'inia kwenye kamba kati ya boti na ufukwe wa Italia huku walinzi hao wakijaribu kuwasaidia.

Tukio hili linakuja baada ya Papa Benedict kuwaomba Wakatoliki kuwa wavumilivu zaidi kwa wakimbizi wanaotoka Afrika Kaskazini.

Aliwaambia waumini katika mji mmoja wenye bandari kwamba Wakatoliki wanafaa kuwakaribisha na kuwa wakarimu kwa maelfu ya wageni wanaowasili kwenye bandari zao mwaka huu.

Idadi ya wakimbizi kutoka Afrika Kaskazini imezidi kwa sababu ya ghasia katika nchi za eneo hilo.

Jana usiku meli ya wavuvi iliyobeba mamia ya watu kutoka Libya iligonga mwamba, ilipojaribu kutia nanga katika kisiwa cha Utaliana cha Lampedusa.

Taarifa zinasema abiria wote walinusurika, na wengine walisaidiwa walinzi wa mwambao wa Utaliana.