Triesman adai wajumbe wa FIFA walitaka rushwa

Lord Triesman Haki miliki ya picha
Image caption Lord Triesman

Shirikisho la soka duniani FIFA limeahidi kufanya uchunguzi juu ya madai ya ukiukwaji wa maadili dhidi ya wajumbe sita wa kamati yake kuu.

Madai hayo yalitolewa kwa ushahidi ulowasilishwa kwa kamati teule ya bunge juu ya michezo nchini Uingereza ambapo aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha soka nchini Uingereza FA David Triesman alidai kuwa wajumbe hao wa Fifa walidai rushwa kama sharti la kuipigia kura England kuwa mwandalizi wa kombe la dunia.

Lord David Triesman alitoa madai hayo mbele ya kamati ya bunge alipotakiwa kueleza kwa nini England ilishindwa kupata kura za kuandaa kombe la dunia mwaka 2018.

Lord Triesman alisema mmoja wa wajumbe alitaka apewe dola milioni nne,huku akitoa madai dhidi ya mjumbe mwengine wa Paraguay Nicolas Leoz ambaye alitaka atambuliwe kwa kupewa cheo cha hadhi na Uingereza.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Sepp Blatter

Mapema kamati hiyo ilisema kuwa itachapisha ushahidi wote kutoka kwa gazeti moja ukidai kuwa wajumbe wawili wa bara Afrika,Issa Hayatou na Jacques Anouma walilipwa dola milioni moja unusu na taifa la Qatar ili waweze kuwapigia kura wapate kuandaa michuano ya mwaka 2022.

Rais wa FIFA Sepp Blatter ametaka kamati ya bunge kuwapa ushahidi huo akisema ni baada tu ya kupokea ushahidi huo ndiyo wataweza kufanya uchunguzi.

Lakini wakati akitoa hakikisho hilo hakuwatetea moja kwa moja wajumbe hao wa kamati kuu ya FIFA akisema ni vigumu kubaini ikiwa wote walikuwa na nia njema au la.