David Haye amuita Klitscho "laghai"

David Haye amembandika jina la "laghai" Wladimir Klitschko katika mkutano na waandishi wa habari mjini Hamburg wakati wa mchakato wa kutangaza pambano lao la ubingwa wa dunia wa kuunganisha mataji.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Klitscho na Haye

Haye Muingereza anayeshikilia mkanda wa ubingwa wa dunia unaotambuliwa na WBA, atakabiliana na Klitscho raia wa Ukraine bingwa dunia wa uzito wa juu unaotambuliwa na IBF na WBO katika ukumbi wa Imtech Arena tarehe 2 mwezi wa Julai.

"Nimeona mtindo wake na kushuhudia anavyofanya ulingoni ni laghai tu," alisema Haye mwenye umri wa miaka 30.

Haye awali alipangiwa kupambana na Klitschko mwezi wa Juni mwaka 2009, alilazimika kujitoa baada ya kuumia, lakini Muingereza huyo ameongeza "miungu wa masumbwi wameamua tarehe 2 Julai ndiyo nitatawazwa kuwa bingwa wa dunia kwa kuunganisha mikanda yote mitatu".

"Nimeaangalia macho ya Klitschko kwa dakika 20 na nimegundua nitamuangamiza," aliongeza Haye, ambaye ameshashinda mapambano 25 kati ya 26.

"Nimetazama macho yake kwa makini na nimemuona amekwishapigika na kuvunjika moyo. Hajawahi kupigana na bondia yeyote mwenye uwezo kama wangu, hili ni jimbo jipya kwangu na kwake.

"Atafanya kile anachokifanya mara zote. Nimekwishapigana na watu wa aina hii, akimuita mpinzani wake 'robots' siku za nyuma- Hwajawahi kunipiga katika kiwango cha ngumi za ridhaa ama za kulipwa, kutoka mabondia wa Ulaya mashariki na hilo halitabadilika kamwe, aliendelea kujigamba Haye.

"Ana ngumi kali, nimekwishashuhudia akiwaumiza watu na ngumi hiyo, lakini siamini kama pambano letu litafika hadi raundi ya 12.

Akizidisha majigambo Haye alisema alikwenda Paris na akafanikiwa kumchapa bingwa wa uzito wa cruiser Jean Marc Mormeck, akaenda Ujerumani akamtandika bondia mwenye umbo kubwa Nikolay Valuev, ambaye amesema Wladimir na kaka yake Vitali wamekuwa wakimkwepa kwa miaka kadha.

Akijibu tambo hizo za maneno, Klitschko, mwenye umri wa miaka 35, alitaka kushikana mkono na Haye lakini Muingereza huyo akakataa na Klitscho akaahidi "atamfunza somo la adabu" Haye tarehe 2 Julai.

"Ninamuheshimu sana, ni bondia hodari akiwa na rekodi nzuri," alisema Klitschko. "Ana makonde mazito na kasi kubwa pamoja na hamasa na safari hii mvuke unatoka katika masikio yake kwa sababu ana hasira na nadhani nitatawala ulingo.

Klitscho aliongeza:"Nitahakikisha najiandaa ipasavyo kwa pambano hili. David Haye atakuwa mtu wangu wa 50 kwenda chini kwa knockout. Mabondia 49 tayari walisalimu amri kwa knockout katika miaka 15 iliyopita na David Haye amewavunjia heshima wote hao.