Wapiganaji wa Gbagbo 'waliwachinja raia'

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ivory Coast

Watu takriban 200 wengi wao raia wameuawa na wapiganaji na mamluki wa rais aliyeondolewa madarakani Laurent Gbagbo, maafisa wamesema.

Mauaji hayo yalitokea wiki iliyopita katika jamii ya watu wanaoishi pwani wakati wapiganaji hao wakielekea mpakani mwa nchi hiyo na Liberia, idara ya Ulinzi ilisema.

Madai hayo hayajathibitiswa na vyanzo huru.

Bwana Gbagbo wiki iliyopita alikuwa anahojiwa kuhusu tuhuma ya vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu

Alikamatwa mwezi mmoja uliopita baada ya kutaa kukubali kushindwa kwenye uchaguzi wa November 2010 .

Rais Alassane Ouattara aliapishwa rasmi wiki iliyopita na anajaribu kurejesha hali ya kawaida baada ya machafuko ya miezi minne ambayo inakadiriwa watu 3,000 waliuawa.

Mauzo nje ya Kakao yalirejea tena na kuifanya Ivory Coast kushika nafasi ya kwanza tena ya uuzaji wa zao hilo duniani mwishoni mwa wiki, maafisa walisema.

"Mamluki wa kulipwa na rais wa zamani Laurent Gbagbo, walitokea Liberia na wapiganaji wa Ivory Coast," Waziri wa Ulinzi alisema katika taarifa iliyosainiwa na Waziri Mkuu Guillaume Soro, ambaye pia ni waziri wa ulinzi.

"Baada ya kuondolewa walielekea kwenye makazi yao" alisema."

Baada ya kukimbia mji mkuu Abidjan, wapiganaji hao walipitia eneo la makazi ya jamii za pwani zikiwemo za Irobo, Grand Lahou, Fresco na Sassandra mahali mauaji hayo yalipotokea" ilisema taarifa hiyo.

Wengi wa waliouawa walichaguliwa kwa kufuata makabila yao au kama waliishi maeneo ambayo yanamuunga mkono Rais Ouattara" ilisema.

Awali mkuu wa kitengo cha Haki za Binadamu cha Umoja wa Mataifa nchini Ivory Coast Guillaume Ngefa alisema miili 68 ya wanaume ilipatikana katika kaburi la pamoja katika eneo la Yopougon, wilaya ya mwisho ya Abidjan kuendeleza utii wake kwa rais wa zamani Gbagbo.

Walisema mauaji hayo yalifanyika siku moja tu baada ya Gbagbo kukamatwa na wanaomuunga mkono Rais Ouattara.