Issa Hayatou akanusha hakuchukua rushwa

Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika Issa Hayatou "amekanusha" kuuza kura yake ya turufu ya Kombe la Dunia kwa Qatar.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Issa Hayatou

Tuhuma hizo zilielekezwa kwake siku ya Jumanne wakati Bunge la Uingereza lilipokuwa likiendesha uchunguzi wa kwa nini England ilishindwa kupata nafasi ya kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia ya mwaka 2018.

Pamoja na Jacques Anouma wa Ivory Coast, Issa Hayatou, wametuhumiwa kupokea dola milioni 1.5 kwa ajili ya kuipigia kura Qatar ifanikiwe kuandaa mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika mwaka 2022.

Hayatou amezielezea tuhuma hizo dhidi yake katika mtandao wa Caf, kuwa ni "za kubuni" tu.

Madai ya tuhuma hizo yametolewa kutokana na ushahidi wa gazeti la Sunday Times ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa kamati ya Bunge.