Kiongozi wa upinzani arudi Uganda

Kizza Besigye
Image caption Besigye alipokuwa Kenya

Kiongozi mkuu wa siasa za upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, amerudi nchini Uganda, baada ya kudai awali kwamba serikali ilikuwa inamzuia kurudi kwa ndege ya shirika la Kenya Airways, alipokwenda kupata matibabu mjini Nairobi.

Makundi ya watu wanaomuunga mkono walimkaribisha Besigye alipopitia barabara za mji.

Besigye alisafiri kwenda Nairobi kutibiwa majeraha aliyoyapata kutokana na gesi ya kutoa machozi na vile vile alipuliziwa pilipili machoni katika rabsha iliyotokea wakati maafisa wa usalama walipomkamata.

Hayo yakiendelea, Rais Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 25, saluti ya mizinga 21, huku akishangiliwa na maelfu ya watu katika sherehe ya kumwapisha.

Viongozi wa mataifa jirani ya Kenya, Tanzania, Sudan ya Kusini, Nigeria, Congo, Ethiopia na Zimbabwe walikuwepo katika sherehe hiyo. Museveni inaelekea alikuwa anazungumza juu ya Besigye, aliposema wapinzani wanataka kusababisha fujo, lakini 'njama zao za kuvuruga' hazitafanikiwa.

Museveni pia alisema Uganda itaanza kutoa mafuta katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, na haitahitaji tena mafuta kutoka ng'ambo.