Matatizo yakithiri Burkina Faso

Burkina Faso ni nchi imetia hali ngumu tangu kuuawa kwa kiongozi wake aliyependwa, Thomas Sankara katika mapinduzi ya kijeshi miaka ishirini iliyopita.

Hata hivyo juhudi zote zilizochukuliwa na mrithi wake na vilevile wakati mmoja rafiki mkubwa, Blaise Compaore hazijazaa matunda yoyote.

Hali iliyopo wakati huu ya ghasia ilianza mwezi febuari mwaka huu kwa mfululizo wa majaribio ya kuipindua serikali, likiwemo lililofanywa na walinzi wa Rais na mara nyingi yakimalizika kwa ghasia za kupindukia.

Image caption Rais Compaore wa Burkina Faso

Akifahamu vyema uwezo wa walinzi wa Rais na ushahid ulio bayana wa jinsi wanavyoweza kusababisha mageuzi ya kiongozi, Rais Compaore hakusita kuitikia madai yao ya nyongeza ya mishahara.

Akionyesha shaka juu ya vuguvugu la mwamko ulioanzia Arabuni kusambaa hadi nchini mwake, kiongozi huyo alimfuta kazi mkuu wa majeshi na polisi kisha akafanya mabadiliko ya baraza lake la Mawaziri.

Alimchagua Waziri mkuu mpya ili kuleta mabadiliko katika serikali ya iliyohudumu kwa kipindi kirefu na kuonekana kama iliyochoka.

Mapema siku ya jumatatu, walimu kote nchini Burkina Faso walianza mgomo wa kudai marupurupu. Wanafunzi nao wakawaunga mkono walimu wao.

Katika mji mkuu Ouagadougou, imearifiwa kuwa wanafunzi walichoma tairi za magari barabarani na kusababisha uharibifu wa majengo.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption wanafunzi walisababisha uharibifu

Makundi ya vijana waliojaa ghadhabu waliandamana katika miji minne mikubwa nchini humo ukiwemo wa pili kwa ukubwa, Bobo Dioulasso. Katika mji wa kusini wa Gaoua, shahidi mmoja wa tukio aliiambia BBC kuwa makao makuu ya chama tawala na mali kutoka makao ya Rais zilichomwa.

Kwa sasa walimu wamefikia mapatano na serikali ya Burkina Faso kumaliza mgomo.

Serikali imekubali kutimiza matakwa ya shirika la walimu la mishahara mkubwa zaidi.

Mapema wiki hii, mwandishi wa BBC katika mji mkuu aliarifu kuwa kundi jingine la askari liliingia mitaani likifyatua risasi angani. Safari hii wakidai mshahara sawa na ule waliopewa walinzi wa Rais.

Kwa mujibu wa mhariri wa idhaa ya Kifaransa ya BBC, Mahamat Adamou, idhaa iliyojulikana kama BBC Afrique, anasema kuwa ukizingatia msimamo wa jeshi ambalo hadi sasa halijawasilisha madai ya kisiasa na bado linamtii Bw.Compaore hana wasiwasi ya kupinduliwa.

Pamoja na hayo upinzani ni mlegevu, umegawanyika na umeshindwa kutumia fursa hii ya ghasia kuonyesha uwezo wake.

Kiongozi huyo ana sifa ya kushiriki mapinduzi yaliyomuwezesha kuingia madarakani kwa kumpindua rafiki yake na hivi kushika wadhifa wa Wizara ya Ulinzi kuna maana kwamba anaweza kuamuru vikosi kuzima aina yoyote ya fujo au jeuri kutoka kwa yeyote au kundi lolote.