Sita wakamatwa na dola milioni 3

Watu sita wakiwa ni wageni nchini Somalia wamekamatwa baada ya kuwasili mjini Mogadishu wakiwa na dola taslimu milioni tatu na laki sita $3.6m kwa mujibu wa polisi ya Somali.

Raia watatu wa Marekani, wa Kenya wawili na Muingereza mmoja walitiwa mbaroni katika mji mkuu wa nchi hiyo.

Msemaji wa Polisi ameiambia idhaa ya Kisomali ya BBC kuwa upelelezi unaendelea kufanywa bila kutoa maelezo zaidi.

Habari ambazo hazijathibitishwa zinasema kuwa huenda fedha hizo ni kwa ajili ya kulipia kikombozi kwa maharamia wanaoendesha shughuli zao kutoka Somalia, ingawa wengi wanaishi maeneo ya kaskazini ya nchi.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Shughuli za utekaji nyara zafanywa kaskazini Somalia

Shirika la Habari la Ufaransa AFP limemnukuu afisa usalama mmoja akisema kuwa ndege moja ilitua mjini Mogadishu, ambako pesa hizo zilitakiwa kuwekwa kwenye ndege nyingine kuzifikisha mahali kwingine.

Raia wa magharibi waliokamatwa ni wazungu wasiokuwa na asili ya Kisomali.

Kwa zaidi ya miaka 20 nchi ya Somalia haina serikali imara na hivyo kusababisha tabia mbovu za ubadilishanaji fedha kwa njia za magendo, uharamia na makundi ya wapiganaji yamekithiri nchini humo. Serikali ya mseto inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa inakabiliana na kundi la Al Shabab lenye uhusiano wa karibu na Al Qaeda.

Kundi hilo pamoja na mengine yanadhibiti maeneo mengi ya kusini na kati ya Somalia.

Wajumbe wa Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa wanatazamiwa kukutana mjini Nairobi na viongozi wa Somalia kuhusu majaliwa ya nchi yao.

Nchi zinazotowa misaada zinashangazwa na mvutano wa madaraka baina ya Rais Sharif Sheikh Ahmed na Spika wa bunge Hassan Sheikh Adam. Muhula wa Rais Ahmed unakaribia kumalizika mwezi Agosti.

Yeye anataka kuongezea mda wake huku Spika akitoa hoja kuwa ni wajibu wa wabunge kumchagua Rais mpya wa serikali hiyo.