Rais Museveni wa Uganda alaani upinzani

Rais Yoweri Museveni
Image caption Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, amelaani vikali kampeni za hasimu wake wa kisiasa Dr.Kizza Besigye za kulalamikia ongezeko la gharama za maisha nchini humo.

Kupitia tahariri yenye kichwa mtawafahamu kwa matunda yao, iliochapishwa na magazeti nchini Uganda, Museveni amesema Besigye alinuia kuangamiza serikali kwa kutumia kampeini hiyo ya kutembea kwa miguu kuenda kazini.

Aidha ametoa onyo kali kwa vyombo vya habari nchini humo na kimataifa likiwemo shirika la BBC, Aljazeera, NTV na Gazeti la Daily Monitor akivilaumu kwa kuegemea upande wa wale ameaita wasio wajibika na maadui wa Uganda.

Kiongozi huyo amesema kwamba vyombo vya habari vitashughulikiwa kama adui.

Maelezo hayo aliyoyandika yamkin wiki moja baada ya kuapishwa Rais Museveni anawakemea akisema, '' kama sio nyinyi mnao ongoza Uganda, kwa sababu raia waliwakataa katika uchaguzi, ni lazima muharibi uchumi wa Uganda?''

Kiongozi huyo anaendelea kuhoji, "kwa nini mshambulie wale ambao hawakuwapigia kura?''

Rais Museveni pia amemshutumu Dr Kizza Besigye na wenzake kwa kupanga njama ya kutumia watu aliowaita wavutaji bangi na kusema kuwa wanakodisha makundi ya kihuni kuharibu mali ya raia.

Rais Museveni amesema chama chake cha NRM kimeanza mchakato wa kutafuta mabadiliko katika katiba ya nchi.

Chama hicho kinapedekeza sheria kali ambapo wauaji, wabakaji na wanaofanya fujo hawatapewa dhamana hadi baada ya kukaa kizuizini kwa kipindi cha muda wa miezi sita.