Uchaguzi wa mabaraza Afrika Kusini

bango la picha ya rais Zuma
Image caption bango la picha ya rais Zuma

Uchaguzi wa mabaraza ya miji unaoanza leo nchini Afrika Kusini una umuhimu mkubwa, kwa sababu unachukuliwa kama mtihani wa umaarufu wa chama kinachotawala cha ANC.

Kuna upinzani mkali na ghadhabu kutoka kwa raia maskini wanaoishi nchini humo.

Raia weusi maskini ambao ndio wengi wanadai chama cha ANC kimeshindwa kuwapa maji, umeme, huduma za afya na mfumo wa elimu unaofanya kazi. Chama hicho kinashutumiwa kwa kuongezeka kwa ufisadi na kushindwa kukabiliana na ongezeka la watu wasiokuwa na ajira pamoja na umaskini.

Chama cha ANC tangu jadi hutegemea raia hao weusi kuwapigia kura. Lakini katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakifanya maandamano yakilenga chama cha ANC kwa kushindwa kuwasaidia watu maskini.

Chama cha ANC pia kinakabiliwa na upinzani kutoka kwa chama cha Democratic Alliance, ambacho kimejitolea kupata kura nyingi kutoka kwa raia weusi.

Chama cha Democratic Alliance kina wafuasi wengi katika eneo la Western Cape, huku Cape Town ukiwa mji muhimu wa mkoa huo.

Chama cha ANC kingependa kubakia mamlakani na kimekua kikiwavutia wapigaji kura kutumia uhusiano wa historia ya nchi hiyo na wapigaji kura weusi ili kuvuta hisia za wengi- kwamba ANC ndicho chama kilichopigania uhuru wao kutoka kwa enzi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Iwapo chama cha ANC hakitafanya vyema katika uchaguzi huu, basi rais Jacob Zuma atakuwa mahali pabaya huku uchaguzi wa chama hicho ukitarajiwa kufanyika mwaka ujao.

Raia wengi wa Afrika Kusini wameamua kususia uchaguzi huo na huenda watu wengi wasijitokeze siku ya upigaji kura na hiyo itachukuliwa kama kupungua kwa umaarufu kwa Bw Zuma na chama chake cha ANC.