Israili yapinga pendekezo la Rais Obama

Benjamin Netanyahu Haki miliki ya picha AP
Image caption Waziri Mkuu wa Israili Benjamin Netanyahu.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amepinga pendekezo la rais wa Marekani Barack Obama kuwa Jamhuri ya Palestina lazima iundwe kuzingatia mipaka iliyochorwa mwaka wa 1967.

Katika hotuba muhimu ya serikali ya Marekani, Bw Obama amesema ''makubaliano ya kubadilisha mipaka kwa haraka'' yatasaidia kuunda Palestina salama .

Lakini Bw Netanyahu amesema mipaka hiyo, ambayo ilikuwepo kabla ya vita vya 1967, katika Mashariki ya kati hayawezi kulindwa.

Bw Netanyahu amajiandaa kukutana na Bw Obama kwa mazungumzo katika Ikulu ya White House.

Takriban raia wa Israel 300,000 wanaishi katika makazi waliojenga katika ukingo wa magharibi mwa mto Jordon, ambayo yako nje ya mipaka hiyo.

Makazi hayo yamejengwa kinyume na sheria za kimataifa, japo Israel inapinga hilo.

Katika hotuba yake, ya sera za Marekani katika Mashariki ya Kati, Rais Obama amesema msingi wa mazungumzo ya amani ni kuunda Palestina mpya na yenye salama.

Bw Obama amesema, ''Marekani inaamini kuwa matokeo ya mashauriano yanapaswa kuwa nchi mbili, huku Palestina ikiwa na mipaka ya kudumu kati yake na Israel, Jordon na Misri''.