Nato yashambulia meli za kivita za Libya

Haki miliki ya picha
Image caption Mashambulio ya anga kwenye meli za kivita za Libya

Majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya Nato yameshambulia kwa anga meli za kivita nane zinazomilikiwa na jeshi la Kanali Muammar Gaddafi katika uvamizi uliofanywa mjini Tripoli, Al Khums na Sirte.

Katika taarifa iliyotolewa, msemaji alisema Nato lazima ichukue "hatua madhubuti" kuzingatia kuongezeka kwa matumizi ya meli za kijeshi kushambulia raia.

Moto na moshi ulikuwa ukishuhudiwa kutoka kwenye meli zilizoshambuliwa kwenye bandari iliyopo kwenye mji mkuu.

Wakati huo huo, kiongozi wa waasi wa Libya ameomba msaada wa kimataifa kwenye miji iliyo milimani magharibi mwa Tripoli.

Taarifa iliyotolewa na muungano huo wa kijeshi ilisema mashambulio yaliyofanywa siku ya Ijumaa yameonyesha kuwa Nato " ina nia ya kuwalinda raia wa Libya, kwa kutumia nguvu zinazostahili na kwa kiwango kinachofaa."

Naibu kamanda wa Nato nchini Libya, Admeri Russel Harding alisema, "Meli zote zilizolengwa jana usiku zilikuwa za kivita bila kifaa chochote cha raia kushambuliwa."

Haijafahamika kama kuna yeyote aliyeuawa.