Sudan Kaskazini yateka Abyei

Jeshi la Sudan Kaskazini limeuteka mji mkuu wa jimbo la mpakani baina ya Sudan Kusini na Kaskazini.

Image caption Mji wa Abyei ulivyoteketezwa

Sudan Kusini itajitenga na Kaskazini mwezi wa July, lakini hatima ya jimbo la Abyei haijulikani. Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liko nchini Sudan, na sasa litashughulika na tatizo hilo lilozuka.

Sudan Kusini imesema uvamizi wa Sudan Kaskazini ni kitendo cha vita.

Rais Omar el Bashir ameifuta kazi halmashauri iliyokuwa ikiongoza Abyei, na hivo kuonesha kuwa jimbo hilo sasa liko chini ya maamlaka ya Kaskazini.

Abyei ilikuwa ikitawaliwa na halmashauri iliyoshirikisha wa-Kaskazini na Kusini, na ikiongozwa na mtu kutoka Kusini.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanaozuru Sudan hivi sasa, wakipanga kwenda Abyei kesho, lakini sasa safari hiyo imevunjwa.

Jeshi la kaskazini liliiteka Abyei mara moja.

Mvutano juu ya Abyei umekuwa ukizidi tangu kura ya maoni iliposhindwa kufanywa katika jimbo hilo mwezi Januari, kuamua hatima yake.

Jimbo hilo linadaiwa na kabila la Sudan Kusini la Dinka Ngok, na wachungaji wa kaskazini, Misseriya.

Haikukubaliwa kuwa Misseriya wana haki ya kupiga kura.

Tangu wakati huo, kumekuwa na wasiwasi, kuwa mapambano yakitokea Abyei, yanaweza kuzusha vita tena baina ya Kusini na Kaskazini.

Baada ya mapigano ya siku mbili, jeshi la kaskazini liliingia mjini na vifaru na kufanya shambulio moja la ndege.

Linasema sababu ni kuwa watu wao 22 waliuwawa, walipoviziwa na kushambuliwa na Sudan Kusini siku ya Alkhamisi.