Wanajeshi kusalia eneo la Abyei-Bashir

Susan Rice Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Susan Rice

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Bi Susan Rice, amesema Umoja huo umepokea ripoti za kutisha kuhusu uporaji wa mali na uteketezaji wa mali katika jimbo la Abyei nchini Sudan, baada ya eneo hilo kutekwa na wanajeshi wa utawala wa Khartoum wiki iliyopita.

Akiongea katika mji mkuu wa eneo la Sudan Kusini, Juba, Bi Rice amesema idadi kubwa ya watu wamekimbia makaazi yao tangu uvamizi huo na kwa sasa wanaelekea eneo la Sudan Kusini chini ya mazingira magumu na hatari kwa usalama wao.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Sudan

Awali rais wa Sudan, Omar al Bashir, alisema wanajeshi wake walijibu uchochezi kutoka kwa wanajeshi wa eneo la Kusini na kwamba wanajeshi hao hawataondolewa kutoka eneo hilo la Abyei.

Serikali za Sudan Kusini na Kaskazini zinadai umiliki wa eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na inakisiwa kuwa mzozo huo wa umiliki wa Abyei unaweza kusababisha vita kati ya pande hizo mbili hasa baada ya Sudan Kusini kutangazwa nchi huru hapo Julai mwaka huu.