Wenye silaha Sudan 'wachoma moto Abyei'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wakimbizi wakiukimbia mji wa Abyei

Majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan yamesema mji unaozozaniwa uliopo mpakani Abyei umechomwa moto tangu ulipotekwa na majeshi kutoka kaskazini.

Ujumbe wa umoja huo umesema umelaani vikali uporaji na uchomaji moto.

Umesema majeshi ya Sudan, yanayoitii serikali ya kaskazini, yalikuwa na jukumu la kuhakikisha sheria inafuatwa Abyei.

Takriban wakazi 20,000 wameukimbia mji huo katika siku za hivi karibuni.

Abyei umekuwa na hali ya wasiwasi mkubwa tangu upande wa kusini kupiga kura mapema mwaka huu kutaka kujitenga na upande wa kaskazini.

Baraza la usalama la umoja wa mataifa linatarajiwa kujadili mtafaruku huo na Rais wa Sudan kusini.