Waasi wa Libya wafungua ofisi Marekani

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Bw Jeffrey Feltman

Waziri mdogo wa Marekani Jeffrey Feltman amesema waasi wa Libya wamekubali mwaliko wa kufungua ofisi mjini Washington.

Bw Feltman ni mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani kuwatembelea waasi hao kwenye mji wa Benghazi.

Marekani imesisitiza kwa kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi kuachia madaraka, lakini haijawatambua moja kwa moja.

Ziara hiyo imefanyika baada ya ndege za majeshi ya umoja wa nchi za kujihami za Ulaya Nato kufanya mfululizo wa mashambulio kwenye mji mkuu wa Libya, Tripoli, mashambulio mazito kutokea mpaka sasa.

Maafisa wa Libya walisema watu watatu walifariki dunia na wengi kujeruhiwa katika shambulio lililofanyika kwenye kambi za jeshi.

Nato ilisema imerusha mabomu kwenye ghala la magari lililopo karibu na ngome ya Bab al-Aziziya ya Kanali Gaddafi uliotumiwa na majeshi yake katika mashambulio iliyofanywa dhidi ya raia.

Hata hivyo, serikali ya Libya imeielezea kama kituo cha kuhifadhi vifaa vya jeshi na waliouawa ni raia.