Man United kumsajili kipa David de Gea

Meneja wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amethibitisha klabu hiyo inakaribia kumsajili mlinda mlango wa Atletico Madrid, David de Gea.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption David de Gea

Manchester United inahitaji mlinda mlango wa kuchukua nafasi ya Edwin van der Sar, anayestaafu soka mwishoni mwa msimu huu.

"Tumekuwa tukilifanyia kazi suala hili la kumpata de Gea kwa muda mrefu sasa," alisema Ferguson.

"Ni kijana mdogo, mwepesi sana, anautulivu langoni na ni mlinda mlango bora kumrithi Van der Sar."

De Gea ameshaidakia Atletico Madrid ya Hispania michezo 45 msimu huu, akiwa amecheza vizuri bila kufungwa michezo 24 hali iliyosaidia klabu yake kumaliza nafasi ya saba katika msimamo wa La Liga.

Hata hivyo bado hajawahi kuichezea timu ya taifa ya Hispania.

Msimu uliopita, aliisaidia Atletico kunyakua kombe la ubingwa wa Ligi ya Europa League walipoilaza Fulham mabao 2-1.

Akijibu taarifa hizo za Manchester United kukaribia kumyakua De Gea, Rais wa Atletico Enrique Cerezo, amekiambia kituo cha radio cha Hispania, Cadena Ser: "Hatufahamu chochote hadi sasa.Hatujafahamishwa rasmi na Manchester United au mchezaji mwenyewe.

Inasemekana mchezaji huyo atachukuliwa kwa kitita cha euro milioni 25 sawa na paundi milioni 22 za Uingereza.

Huku mkataba wake ukiwa unamalizika mwaka 2013, Atletico ina matumaini ya kumshawishi De Gea kusaini mkataba mwengine, lakini mlinda mlango huyo amesema atatoa uamuzi juu ya mustakabali wake itakapofika mwisho wa mwezi wa Juni.