Ratko Mladic akamatwa Serbia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ratko Mladic

Ratko Mladic, anayesakwa na waendesha mashtaka wa umoja wa mataifa kwa uhalifu wa kivita wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Bosnia katika miaka ya 90, amekamatwa Serbia na anapelekwa the Hague.

Rais wa Serbia Boris Tadic amethibitisha kukamatwa kwa aliyekuwa mkuu wa jeshi wa Serb wa Bosnia katika mkutano na waandishi wa habari.

Jenerali Mladic anatuhumiwa kwa mauaji ya takriban Wabosnia 7,500 wa Kiislamu wanaume na vijana wa kiume huko Srebrenica mwaka 1995.

Ni miongoni mwa washukiwa maarufu wa uhalifu wa kivita aliyekuwa akitafutwa tangu kukamatwa kwa Radovan Karadzic mwaka 2008.

Rais Tradic alisema tayari kulikuwa na mipango ya kumsafirisha Jenerali Mladic kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita The Hague, na baadae taarifa zilisema kuna ndege iliyomchukua mshukiwa huyo huko Belgrade kuelekea Uholanzi.