Ziara ya Zuma Libya 'haijahitimishwa'

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waliojiondoa kwenye jeshi la Kanali Gaddafi

Mazungumzo baina ya Rais wa Afrika Kusini na kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi mjini Tripoli imemalizika bila kuwa na tangazo lolote kuelekea kumalizika kwa mgogoro wa Libya.

Bw Jacob Zuma alisema Kanali Gaddafi atakubali kusitisha mapigano lakini hatoondoka madarakani, kama inavyotakiwa na majeshi ya Nato na waasi wa Libya.

Pendekezo la kusitisha mapigano lilikataliwa mwezi uliopita baada ya ujumbe wa upatanishi uliofanywa na Bw Zuma kwa niaba ya Umoja wa Afrika.

Msemaji wa waasi wa Libya amepuuzilia mbali wito wa kusitisha mapigano, na kuahidi kuendelea na mapigano.

Waziri wa mambo ya nje wa Italia Franco Frattini anatarajiwa kutembelea eneo linalodhibitiwa na waasi wa Benghazi siku ya Jumanne.

Bw Frattini atakutana na wanachama wa Baraza la Mpito la Taifa la Libya, muungano wa upinzani dhidi ya Kanali Gaddafi.

Ziara yake hiyo inafanyika baada ya kuwepo mkutano wa waandishi wa habari mjini Rome ambapo maafisa waandamizi wa kijeshi wanane wa Libya walipotangaza kujitoa kwenye majeshi ya Kanali Gaddafi.