Rwanda yataka maiti za watu zifukuliwe

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mafuvu ya waliokufa kutokana na mauaji ya kimbari

Chama cha upinzani nchini Rwanda kimeishutumu serikali ya nchi hiyo kwa kuwalazimisha watu kufukua miili ya ndugu zao waliouawa wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ili iwekwe kwenye eneo la maonyesho ya kumbukumbu.

Serikali imesema mabaki ya miili iwekwe pamoja katika maeneo hayo ili watu waisahau mauaji ya maelfu ya Watutsi na Wahutu waliokuwa wakifuata siasa za wastani.

Mwakilishi wa chama cha upinzani cha Rwandan National Congress, Jonathan Musonera amesema yeye binafsi ameathiriwa na amri hiyo ya serikali.

Alisema serikali iliamrisha wafukue miili ya jamaa zao na ipelekwe katika makumbusho ya mauaji ya kimbari.

Familia yangu ilikataa lakini serikali ilitishia kuamrisha wafungwa waifukue miili hiyo, hatukuwa na la kufanya isipokuwa kwa jamaa zetu kufukua miili hiyo na kuipeleka katika makumbusho ya mauaji ya kimbari.

Bw Musonera aliongeza kwamba familia yake imesononeshwa sana na amri hiyo akisema walipoteza ndugu zao kwa njia ya kikatili.

Walistahili kupewa mazishi ya heshima, kilichotokea hakiaminiki, kwani alikuwa na uhusiano wa upendo wa hali ya juu kwa wazazi, ndugu, dada na marafiki waliopotea wakati wa mauaji, na kwamba hawezi tena kustahamili kuona mifupa yao ikining'inia maeneo ya makumbusho.

Hata hivyo chama cha manusura wa mauaji ya kimbari ambacho kina fungamano kubwa na serikali kinaunga mkono sera hiyo ya kufukua miili.

Jean Pierre Dusingizemungu mkuu wa chama hicho anasema miili ya watu hao inapaswa kuwekwa katika maeneo hayo ili kuonyesha kilichotokea wakati wa mauaji.

Aliongeza miili hiyo inapaswa kuhifadhiwa vizuri ili iweze kuonyeshwa kwa muda mrefu.

Kuna maeneo kadhaa ya kumbukumbu za mauaji ya kimbari nchini Rwanda, kubwa zaidi mjini Kigali ambako kuna mifupa na mafuvu ya watu lakini mawili yanaonyeshwa hadharani.

Serikali ya Rwanda inataka milli ya kila muathiriwa wa mauaji ya kimbari yaonyeshwe hadharani ili kubainisha kiwango cha ukatili wa mauaji hayo.

Lakini wengi wanaoambiwa kufukua miili hiyo ya jamaa zao waliouwawa miaka 17 iliyopita, wangependelea wapumzike kwa amani mahali walikozikwa.