Sudan: '150,000 wakimbia mzozo wa Abyei'

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir

Waziri kutoka kusini alisema, idadi ya watu waliohama kutoka eneo lenye mzozo la Abyei nchini Sudan baada ya kutekwa na majeshi ya kaskazini imefikia 150,000.

Waziri wa masuala ya kibinadamu James Kok Ruea alisema, "Hali ni mbaya- wanakimbia wakihofia ukatili, bila ya msaada wowote."

Mwandishi wa BBC Peter Martell huko Juba amesema kiwango hicho ni kikubwa mno ukilinganisha na makadirio ya umoja wa mataifa ya baina ya watu 30,000 na 40,000.

Wakati huo huo, kaskazini imesema inaweza kuanza mazungumzo juu ya mgogoro huo mwishoni mwa juma.

Mpatanishi wa Abyei kutoka kaskazini, Al-Dirdiri Mohammed Ahmed, aliliambia shirika la habari la AFP kuwa anatumai mazungumzo yatafanyika Ethiopia siku ya Jumamosi ambapo yatasimamiwa na wapatanishi wa Umoja wa Afrika.

Wachambuzi wanahofia mgogoro kwenye mji huo, unaogombaniwa pia na kusini unaotarajiwa kuwa huru mwezi Julai, unaweza kuchochea vita vya kaskazini na kusini ambapo takriban watu milioni 1.5 walifariki dunia.

Siku ya Alhamis, Rais wa kusini Salva Kiir alisema hatowaongoza watu wake kwenye mapigano tena na kaskazini juu ya Abyei na mazungumzo ndio njia bora ya kutatua mgogoro huo.