Watoro wanaokimbia sheria Afrika

Jaji wa Mahakama nchini Serbia ametoa uamuzi kwamba kamanda wa majeshi ya Waserb wa Bosinia Ratko Mladic kwa afya yake anaweza kufikishwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya The Hague.

Amekuwa mafichoni kwa miaka 16 kabla ya kukamatwa kwake siku ya Alhamis.

Lakini, Je watoro wanaotafutwa wa barani Afrika wako wapi? Na kwanini bado wanakimbia mkono wa sheria?

Image caption Bosco Ntaganda

Wengi kati ya wanaotafutwa ni wale inaodaiwa walihusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Kwa mfano mahakama ya jinai ya kimataifa kuhusu Rwanda ICTR ina orodha ya watu tisa .

Wa kwanza kabisa katika orodha hiyo ni Felicien Kabuga, ambae alikuwa ni miongoni mwa matajiri wakubwa nchini Rwanda.

Upande wa mashtaka ulidai kwamba mnamo mwaka 1993 alinunua mapanga laki kadhaa, alikifadhili kikundi cha wanamgambo cha Interahamwe na kusaidia matangazo ya kituo cha redio kilichotumika kuchochea mauaji ya Watutsi.

Upande wa mashtaka unaamini kuwa Felicien Kabuga anajificha nchini Kenya, madai yanayokanushwa vikali na wakuu wa serikali ya Kenya.

Nchini Uhispania Jaji anayewakilisha familia za Wahispania watatu waliokuwa wakitumikia shirika moja la misaada la Hispania waliouawa nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wakati wa mauaji ya Rwanda anatamfuta Justus Majyambere na wengine 39.

Image caption Joseph Kony

Alikuwa ni mfuasi wa kundi la waasi wa Rwanda RPF chini ya rais wa sasa Paul Kagame, na anashutumiwa kuhusika na vitendo kadha vya jinai ikiwemo mauaji ya kimbari.

Justus Majyambere sasa anatumikia jeshi la taifa nchini Rwanda.

Mtoro mwingine anayetafutwa na mahakama ya jinai ya kimataifa kwa vitendo vya uhalifu dhidi ya binadamu ni aliyekuwa kiongozi wa waasi Jean Bosco Ntaganda wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo.

Serikali ya Congo imekataa kumtoa kwa sababu inasema ni mtu muhimu katika juhudi za kutafuta amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Yeye pia sasa ni afisa wa cheo cha Jenerali katika jeshi la taifa.

Nchini Uganda pia kuna mshukiwa wa uhalifu wa kivita. Yeye ni kiongozi wa kundi la Lords Resistance Army , Joseph Kony, ambae inadhaniwa yuko mafichoni katika mipaka ya Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kideokrasia ya Congo.

Anashutumiwa na mahakama ya jinai ya kimataifa kwa kuhusika na jinai katika vita, ikiwemo mauaji, chinjachinnja na kuzuia wanawake kwa minajili ya vitendo vya ngono.