Amnesty International inatimia miaka 50

Shirika la Kimataifa la kutetea haki za kibinaadamu maarufu kabisa, Amnesty International, linasherehekea nusu karne tangu kubuniwa.

Haki miliki ya picha Amnesty

Katika shughuli zake shirika hilo la kujitolea, linajitenga na siasa na masilahi ya kiuchumi na dini, na linagharimiwa kwa michango ya wanachama na wafadhili kati ya jamii.

Sasa lina wafuasi kama milioni tatu katika nchi 150.

Mwaka 1961 wanafunzi wawili wa Ureno walifungwa kwa kusema wanataraji watakuwa huru.

Wakati huo Ureno ikiongozwa na utawala wa kidikteta.

Habari za kufungwa kwa wanafunzi hao kulimchochea wakili mmoja wa Uingereza, Peter Benenson, kuanzisha kampeni ya kupigania wafungwa wanaozuwiliwa kwa sababu ya itikadi zao.

Ndipo shirika la Amnesty likaanzishwa.

Amnesty International, ambayo imewahi kupata zawadi ya amani ya Nobel, sasa inapata michango ya karibu dola 300 milioni kila mwaka, kufanya shughuli zake.

Kazi yake piya ni kujaribu kuondosha adhabu ya kifo, na hivi karibuni, kupambana na chanzo cha umaskini, na kuheshimu haki za raia.

Lakini baadhi ya wadadisi wanasema kwa kujiongezea majukumu, shirika la Amnesty linapoteza shabaha ya lengo lake la asili.