UN:Pande zote zilihusika katika uhalifu wa kivita Libya

Wanajeshi wa Libya Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wanajeshi wa Libya

Wachuguzi wa Umoja wa Mataifa wameshtumu vikosi vya serikali ya Libya kwa uhalifu wa vita na ukatili dhidi ya binaadamu.

Wataalamu wa haki za binaadamu wanasema wamepata ushahidi wa uhalifu ikiwemo mauaji na mateso, katika mfumo ambao unaonyesha kuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi, alifahamu kinachoendelea.

Ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa pia umesema vikosi vya upinzani vilihusika katika ukiukwaji wa haki za binaadamu na hio pia ni uhalifu wa kivita, ingawa matukio yao hayakuwa mengi.

Mapema, shirika la kujihami la nchi za magharibi, NATO, liliongeza muda wake wa kuwa Libya kwa siku 90 zaidi.

Ripoti hio ya wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, iliotolewa siku ya Jumatano mjini Geneva, iliandaliwa na wataalamu watatu wa masuala ya haki za binaadamu.

Mapema siku ya Alhamisi, kulikuwa na taarifa za mashambulio katika mji mkuu Tripoli, huku ndege zikisikika zikipaa angani. Nato imekuwa ikifanya mashambulio ya angani kila mara katika mji mkuu wa Libya.