Sudan yataka UN iondoe vikosi vyake nchini humo

Rais wa Sudan Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais wa Sudan

Serikali ya Sudan imeambia Umoja wa Mataifa rasmi kwamba inataka vikosi vyake vya kulinda amani kuondoka nchini baada ya Sudan Kusini kuwa nchi huru tarehe 9 mwezi Julai.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Ban Ki Moon amependekeza vikosi hivyo viongezwe muda wa miezi mitatu wakati pande hizo zikijaribu kusuluhisha matatizo kati yao.

Ombi hilo la Sudan limekuja wakati hali ya wasiwasi imezidi kati ya Sudan Kaskazini na Kusini kuhusu mipaka.

Balozi wa Sudan katika umoja wa mataifa Daffa-Alla Elhag Ali Osman ameambia baraza la usalama la umoja wa mataifa kwamba hakuna haja ya kuongeza muda kwa vikosi vya kulinda amani,hata kama kutatua na masuala yenye kuleta utata kati yao na Sudan Kusini baada ya wao kuwa huru: Amesema hayo yanaweza kutatuliwa kwa mashauriano.

Lakini afisa mmoja mkuu kutoka Sudan Kusini Ezekiel Gatkuoth,anasema Umoja wa Mataifa lazima iwe na vikosi vyake pande zote. Ameridhishwa na vikosi hivyo kuwa upande wa Kusini akisema muhimu ni kuhakikisha kuwa usalama unaimarishwa.

Lakini akasema kuwa pendekezo la kuwa na wanajeshi wa kulinda amani elfu saba pekee halitoshi.

Haifahamiki namna baraza la usalama litajibu ombi hilo la serikali ya Khartoum.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanajeshi wa Sudan Kusini

Kuwa na vikosi vya kulinda amani upande wa Kusini pekee kutadhoofisha juhudi za kuangalia mpaka kati ya Kusini na Kaskazini,ambako kuna sehemu inayozozaniwa.

Na pia kuna wasiwasi baada ya mauaji ya hivi majuzi katika eneo linalozozaniwa la Abyei,jambo lilosababisha majeshi ya kaskazini kuuteka mji wa Abyei.

Baraza la usalama limetaka serikali ya Khartoum iondoke kwenye eneo hilo,bwana Osman anasema wataondoa majeshi tu iwapo kutakuwa na makubaliano juu ya mkakati wa kisiasa na usalama.

Nchi ya Ethiopia imejitolea kupeleka vikosi vya kulinda amani katika eneo la Abyei,Bwana Gatkuoth amesema utawala wa Sudan Kusini umekubali pendekezo hilo huku Bwana Osman akisema kuwa utawala wa Khartoum bado unatafakari kuhusu wazo hilo.