FAO yachagua kiongozi mpya

Shirika kubwa kabisa la Umoja wa Mataifa, FAO, ambalo linashughulika na chakula, limepata kiongozi mpya, naye ni Jose Graziano da Silva kutoka Brazil.

Haki miliki ya picha ABr
Image caption Jose Graziano da Silva

Amemshinda kwa kura kidogo, waziri wa zamani wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Uspania, Miguel Angel Moratinos katika uchaguzi wa nchi zanachama.

Kiongozi mpya, anachukua nafasi ya Bwana Diouf aliyeongoza FAO kwa miaka 18, wakati bei za vyakula ziko juu, na idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa inazidi kuongezeka.

Shirika la Chakula Duniani, FAO, linamchagua kiongozi mpya leo wakati bei za chakula ziko juu, na idadi ya watu duniani wanaokabiliwa na njaa inazidi kuongezeka.

Jacques Diouf kutoka Senegal ameongoza shirika hilo la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na chakula kwa karibu miongo miwili lakini, kufuatana na sheria mpya, anayemrithi hatoweza kuongoza kwa zaidi ya mihula miwili ya jumla ya miaka 7.

FAO ilianzishwa baada ya Vita vya Pili vya Dunia, ili kuimarisha viwango vya lishe na hali ya maisha duniani.

Hivi karibuni shirika hilo lilionya kuwa bei za vyakula zilifikia kilele mwezi wa Februari na kuwafanya mamilioni ya watu kuishi na njaa.

Watu wenye njaa wamefikia 925-milioni, wengi wao wakiwa nchi zinazoendelea.

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, akizungumza katika kikao cha FAO Rome, aliyalaumu mataifa tajiri kwa kunyakua ardhi kutoka maskini.

Bwana Annan alisema inatia wasi-wasi mkubwa, kuwa ardhi ya kulima ya ukubwa sawa na Ufaransa, ilinunuliwa Afrika mwaka wa 2009 peke yake, na makampuni ya fedha na matajiri.

Alisema siyo haki kwa ardhi ya kulima kuchukuliwa namna hivo, na chakula kusafirishwa nje, wakati kuna njaa katika nchi zenyewe.