Jisr al-Shughour, Syria, inashambuliwa

Mwananchi mmoja wa Syria aliyeshuhudia baadhi ya matukio ya usiku wa Ijumaa, kaskazini magharibi mwa nchi, anasema wanajeshi wa Syria walitumia vifaru kushambulia kijiji karibu na mji wa Jisr al-Shughour.

Haki miliki ya picha AP

Mtu huyo ambaye amekimbilia Uturuki, anasema jeshi liliangamiza mazao ya kijiji.

Ijumaa televisheni ya Syria iliarifu kuwa jeshi liliingia Jisr al-Shughour kurejesha amani.

Shahidi huyo anaeleza kuwa shambulio lilianza alfajiri kabla ya watu kuamka.

Kijiji chake kiko kilomita nne nje ya Jisr al-Shughour, na kiko juu ya kilima.

Aliona shambulio dhidi ya kijiji kilioko chini ya kijiji chake, ambacho anasema, kiliingiliwa na vifaru 40.

Kilizungukwa na wanajeshi waliokuwa na bunduki, na vifaru vilishambulia nyumba, lakini hajui watu wangapi walikufa.

Tena wanajeshi walichoma moto mashamba ya ngano yanayozunguka kijiji na kufyeka mizaytuni.

Shahidi huyo anasema aliona kijiji chake nacho kitakutwa na hatima hiyo hiyo, na aliamua kukimbilia Uturuki pamoja na mkewe, watoto 10 na farasi wake wane.

Iliwachukua saa nne kufika mpakani kwa miguu. Ameiacha familia upande wa Syria wa mpaka, kujaribu kuona kama Uturuki itamruhusu aingie na farasi wake piya.