Hadi akutana na balozi wa Marekani

Waandamanaji wakisheherekea Yemen Haki miliki ya picha 1
Image caption Waandamanaji wakisheherekea Yemen

Naibu wa Rais Saleh, Abd-Rabbu Mansour Hadi, ambaye sasa ni kaimu rais, amekutana na balozi wa Marekani Yemen, Gerald Feierstein, kujadili hali ya siasa nchini.

Mwandishi wa BBC Mashariki ya Kati anasema, ikiwa Rais Saleh ndio ameondoka kabisa, kutaanza kinyang'anyiro chengine kuania madaraka, baina ya mwanawe Rais saleh, makamo wa rais, viongozi wa makabila, na viongozi wa maandamano wanaotaka uongozi.

Katika taarifa zaidi, waziri wa mashauri ya Nchi za Nje wa Uingereza, William Hague, amesema Uingereza imekuwa ikimsihi Rais Saleh akubali maafikiano ili kurejesha utulivu wa Yemen, ambayo alisema ndio unaotia wasi-wasi kwa sababu ya usalama wa Ungereza.

Na kamanda wa kikosi cha Ufaransa Afrika Mashariki, ambaye piya anashughulika na Yemen, ameonya kunaweza kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Jenerali Thierry Caspar-Fille-Lambie, alisema Yemen ikiendelea kutibuka, maharamia wa Kisomali wanaweza kuanza kuendesha shughuli zao katika Ghuba ya Aden, kutoka upande wa Yemen piya.