UN yachunguza mapigano Sudan

Umoja wa Mataifa umesema kuwa unafanyia uchunguzi mapigano yaliyozuka katika eneo linalozalisha mafuta katika jimbo la South Kordofan nchini Sudan.

Image caption Mwanajeshi wa UN Sudan.

Eneo hilo tete liko kaskazini mwa mpaka wa Sudan Kusini lakini linakaliwwa na watu wengi waliopigana kwa niaba ya Sudan kusini katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyomalizika mwaka 2005.

Maswala nyeti

Hali ya wasiwasi imekuwa ikikumba eneo hilo wakati Sudan Kusini ikitazamiwa kujitangazia rasmi uhuru wake kutoka kaskazini kuanzia mwezi Julai.

Maswala nyeti katika mzozo huo yanajumuisha eneo kamili la mpaka kati ya kaskazini na kusini na mustakabal wa jimbo la Abyei linalozozaniwa.

Image caption Ramani ya Sudan

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa watu waliojihami kwa bunduki wamepora silaha kutoka katika kituo cha polisi cha Kadugli, katika mji mkuu wa jimbo la South Kordofan.

Saa chache baadaye kulitokea ufyatulianaji risasi katika kijiji kimoja kilichoko kilomita 48 kutoka mji wa Kadugli.

Haikubainika ikiwa matukio hayo mawili yalikuwa na uhusiano.

Jimbo la South Kordofan linadhibitiwa na serikali ya Khartoum lakini linakaliwa na wanajeshi wengi wanaoegemea upande wa kusini.