Uturuki haitawakataa wakimbizi wa Syria

Ambulensi za Uturuki Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Magari ya kubebea wagonjwa ya Uturuki yakiwasaida waliojeruhiwa Syria

Waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, amesema nchi yake haitafunga mipaka yake kwa wakimbizi kutoka Syria, wakati mamia ya watu wamekuwa wakiitoroka nchi hiyo, kutokana na msukosuko wa kisiasa.

Bw Erdogan amesema anafuatia kwa makini matukio nchini Syria, na amemsihi rais Bashar al Assad kutekeleza mapendekezo ya mabadiliko ya kisiasa.

Mwandishi wa BBC aliye mpakani kati ya Uturuki na Syria ameelezea kwamba magari ya kubebea wagonjwa kutoka Uturuki yamekuwa yakivuka mpaka na kuingia Syria katika siku za hivi karibuni, na kurudi Uturuki yakiwa yamewabeba watu waliojeruhiwa katika maandamano ya kuipinga serikali ya Syria.

Ameelezea pia kuna raia wa Syria ambao wanaonelea badala ya kuvuka mpaka na kuingia Uturuki kama wakimbizi, ni afadhali kuishi katika hema hafifu walizojitengenezea, mita mia chache kutoka eneo la mpakani.