Ban-Ki Moon atafuta tena kuchaguliwa UN

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, ametangaza rasmi kuwa atagombea tena wadhfa huo kwa mhula wa pili..

Bwana Ban ambaye ni raia wa Korea Kusini amesema ataendelea kuuongoza umoja wa mataifa kama chombo cha kujenga daraja katika enzi hii ya mageuzi duniani.

Mwandishi wa BBC wa maswala ya umoja wa mataifa amesema kuna uhakika mkubwa kwamba bwana Ban atachaguliwa tena.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Ban-Ki Moon

Aliwahi kuwa waziri wa mashauri ya nchi za kigeni, Korea Kusini.

Tayari amependekezwa na mataifa ya Ufaransa na Uchina na hana mpinzani yeyote hadi kufikia sasa.

Tangu mwanzo Bw Ban amejitokeza kama mtu anayependelea diplomasia ya upole, ikilinganishwa na mtangulizi wake Kofi Annan.

Katika mkutano na waandishi wa habari mjini New York siku ya Jumatatu Bw Ban alisema: "imekuwa ni fursa kubwa kwangu kuongoza shirika kubwa kama hili.

"ikiwa nitaungwa mkono na mataifa wanachama, itakuwa heshima kubwa kwangu kwa mara nyingine, na katika muda wangu wote nikishikilia hatamu za uongozi, nimejaribu kuwa chombo cha kujenga daraja la upatanishi."

Diplomasia ya 'kimya kimya'

Mataifa yenye uwezo mkubwa katika Baraza la Usalama yaliyonekana kutaka kiongozi anayeendesha mambo yake kimya kimya baada ya masaibu ya vita vya Iraq mwaka 2003.

Bwana Ban ambaye alichukuwa hatamu za uongozi mwaka 2007 alikosolewa kwa kuwa na tofauti nyingi na mataifa hayo yenye ushawishi mkubwa na pia kwa kushindwa kukabiliana moja kwa moja na watu wanaoshutumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu duniani.

Lakini siku ya jumatatu Bw Ban amesisitiza kwa mara nyingine kwamba alikuwa mtetezi mkubwa wa haki za kibinadamu - na kwamba alisifiwa hivi maajuzi kwa kuunga mkono waandamanaji wanaopigania demokrasia katika mataifa ya kiarabu.

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba mafanikio yake katika Umoja wa Mataifa ni pamoja na kusimamia shughuli za kibinadamu wakati wa mikasa mbali mbali iliyoikumba dunia, na pia kushinikiza swala la mabadiliko ya hali ya naga kupewa umuhimu mkubwa na serikali za ulimwengu.

Baada ya kuidhinishwa na mataifa ya Ufaransa na Uchina, wanadiplomasia wanatarajiwa kwamba mchakato wa kuchaguliwa kwake utakuwa umekamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.