Milipuko yarindima Libya

Milipuko mikubwa imetikisa mji mkuu wa Libya, Tripoli, katika mfululizo wa mashambulio ya anga yaliyofanywa na majeshi ya Nato.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Milipuko yatikisa Libya

Baadhi ya milipuko ilionekana kutua karibu kabisa na eneo analoishi kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

Mashambulio haya yamekuja, huku kukiwa na shinikizo la kidiplomasia kumtaka aondoke.

Kiongozi wa ujumbe wa Umoja wa Afrika, rais wa Mauritania Mohammed Ould Abdel Aziz amesema kuondoka kwake ni muhimu ili kumaliza mzozo uliopo.

Urusi na Uchina kwa mara ya kwanza zimepeleka wajumbe wake wa ngazi za juu, katika eneo linalodhibitiwa na waasi la Benghazi, katika jitihada za kusuluhisha na kumaliza mzozo uliodumu kwa miezi minne sasa.

"Tumekuja Benghazi kusaidia mazungumzo kati ya pande mbili," amesema mjumbe kutoka Urusi, Mikhail Margelov.

Wakati huohuo, waziri wa mambo ya nje wa Libya Abdul-Ati al-Obeidi amekwenda Beijing kwa ajili ya mazungumzo ya kile kinachotajwa na wachambuzi kuwa juhudi za kurejesha uhusiano wa kidiplomasia katika ngazi ya Kimataifa.

Kwa upande wa kijeshi, Nato imeendesha mashambulio ambayo aghalabu huyafanya mchana mjini Tripoli, ikiwemo mashambulio katika kambi ya kijeshi karibu na nyumba ya Kanali Gaddafi, katika siku ambayo inadhaniwa kuwa anatimiza umri wa miaka 69.