Siasia asema uchovu uliiponza Nigeria

Kocha wa Nigeria, Samson Siasia, amekiri kuwa sababu ya kikosi chake kupoteza alama muhimu dhidi ya Timu ya Taifa ya Ethiopia wiki iliyopita, ilikuwa ni uchovu baada ya Timu yake kuchuana na Argentina katika mechi ya kirafiki.

Image caption Kocha wa Nigeria Samson Siasia

Mechi hiyo ya kufuzu kwa kombe la Mataifa ya Afrika mwaka wa 2012 ilimalizika kwa suluhu ya 2-2 baina ya Nigeria na wenyeji Ethiopia, na kuiacha timu hiyo ya Super Eagles ikiwa na alama tatu nyuma ya viongozi Guinea inayoongoza Kundi B kukiwa na mechi mbili zilizosalia.

Baada ya kuilaza Argentina 4-1 mjini Abuja Jumatano iliyopita, Nigeria iliwasili mjini Addis Ababa saa chache Kabla ya mechi hiyo kuanza. "Nadhani vijana wangu walichukulia mechi yao na Argentina kuwa muhimu zaidi, hatua iliyosababisha wao kutocheza kwa umakini wakati wa mechi yao na Ethiopia" alisema Sisia.

"hali hii imetufanya sisi kulipa gharama kubwa, kwa kupoteza pointi muhimu sana, pia kulikuwa na tatizo la uchovu miongoni mwa sababu nyingine, lakini tulicheza vyema" kocha huyo wa Nigeria alisema.

Msimamo wa kundi B

Guinea Pointi 10 Nigeria Pointi 7 Ethiopia Pointi 4 Madagascar Pointi 1

Timu hiyo ya Nigeria, imepangiwa kuchuana na Argentina kwa mara nyingine nchini Bangladesh tarehe 6 mwezi Septemba mwaka huu, lakini kocha Siasia amesema lengo lake kuu ni kufuzu kushiriki fainali za kombe la Mataifa ya Afrika.

Image caption Timu ya Taifa ya Nigeria kabla ya mechi yao na Ethiopia

Nigeria imepangwa kuchuana na Madagascar katika michuanao ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika tareh 4 Septemba mjini Dhaka kuchuana na Argentina saa 48 baadaye.

Siasia amedokeza kuwa atafanya mabadiko makubwa katika kikosi chake kitakacho elekea kule Antananarivo ili kuongezea matumaini ya Nigeria ili kufuzu kwa fainali hizo za nchini Gabon na Equatorial Guinea mwaka 2012.